Fedha za shule hii zilitumiwa wapi?

Kulwa Magwa

BADALA ya kupewa sh. 2,110,000 kwa kipindi cha miezi sita, shule ya msingi Sambaru, iliyoko katika wilaya ya Ikungi, mkoa wa Singida, ilipatiwa sh. 350,000 na serikali zikiwa ni malipo ya ruzuku iliyopaswa kutolewa kwa kila mwanafunzi wa shule hiyo.

Fedha hizo ambazo ni ruzuku inayotolewa na serikali, zilifika katika shule hiyo zikiwa pungufu kwa sh. 1,760,000.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulioanzishwa na serikali mwaka 2002, kila mwanafunzi nchini hutengewa sh. 10,000 kwa mwaka.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sambaru, Innocent Macha, alisema ofisini kwake, mwishoni mwa mwaka jana, kuwa walipokea kiasi hicho cha fedha kama mgawo wa Aprili hadi Septemba.

Kwa mujibu wa MMEM shule hiyo yenye wanafunzi 422, ilipaswa kupelekewa sh. 2,110,000 kwa kipindi cha miezi hiyo.

Macha alisema katika kipindi cha Aprili hadi Juni, shule hiyo ilipokea sh. 150,000 – ambapo Juni hadi Septemba ilipatiwa sh. 200,000.  Awali, kati ya Januari hadi Machi, mwaka huo, shule hiyo ilipewa ruzuku iliyostahili ya sh. 1,055,000.

Kutokana na kupewa ruzuku pungufu, ina maana kila mwanafunzi wa shule hiyo alipatiwa sh. 829 kati ya Machi hadi Septemba, badala ya sh. 5,000 kwa kipindi hicho.

maktaba-hakuna

Kutokana na kutokuwepo kwa maktaba na makabati, vitabu huwekwa kwenye maboksi

Kwa mujibu wa MMEM, fedha zinazotumwa shuleni kwa utaratibu huo – hutumika kununulia vitabu vya kiada, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukarabati wa majengo na vifaa vya shule, gharama za utawala na uchapishaji wa mitihani.     

Kulingana na idadi ya wanafunzi, shule hiyo ya msingi katika kipindi cha miezi hiyo sita ilipaswa kupewa ruzuku ya sh. 2,110,000 na kwamba, kwa mwaka mzima ilitakiwa kupelekewa sh. 4,220,000.

Mwalimu Macha alisema kwamba, licha ya utaratibu wa kuzipatia shule ruzuku – kwa maana ya kila mwanafunzi kutengewa sh.10, 000, upatikanaji wa fedha hizo siyo mzuri.

Mwalimu-Mkuu-Sambaru

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sambaru, Innocent Macha

“Uzoefu unaonyesha sana sana shule ikipatiwa fedha nyingi huwa hazizidi robo au chini ya robo ya kiasi inachopaswa kupata, “alisema mwalimu huyo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jumanne Khamis, alisema hajui iwapo ruzuku inayotolewa na serikali kwa kila mwanafunzi ni haki ya msingi kuifuatilia inapochelewa kutolewa au isipotolewa.

Alisema, hata kwenye vikao vya serikali ya kijiji hawajawahi kujadili suala hilo kwa kuwa wanaamini hawana haki ya kujua na kama ingekuwa haki yao kufahamu wangefuatilia fedha hizo wilayani.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata, Jumanne Gwae, alikiri shule hiyo na zingine kwenye kata hiyo kupewa ruzuku pungufu na wakati mwingine hazipelekewi kabisa kwa miezi fulani ya mwaka.

“Hilo wilayani ndio wana majibu nalo, maana haliko Sambaru peke yake – kila shule ukienda utalikuta,”alisema.

Alipofuatwa ofisini kwake kutoa ufafanuzi wa suala hilo na mambo mengine wilayani humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Illuminata Mwenda, alikataa kusema chochote kwa madai kwamba mwenye mamlaka hayo ni mkuu wa wilaya pekee.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Manju Msambya, licha ya kushutumu uamuzi wa mkurugenzi kugoma kuzumgumzia mambo aliyotakiwa na mwandishi wa habari hii, alisema shule nyingi wilayani humo zinakabiliwa na tatizo la kupata fedha za ruzuku kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo.

“Hilo si tatizo la Sambaru au Ikungi peke yake ila ni la kitaifa, nadhani linatokana na upatikanaji wa fedha serikalini ingawa (bajeti) zinapitishwa bungeni,”alisema.

Kwa upande, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema ruzuku kutopelekwa yote katika shule hiyo na nyingine nchini inatokana na serikali kutopenda kuwekeza ipasavyo katika elimu.

Alisema kuna mianya mingi ya wizi wa fedha za umma ambayo iwapo ingezibwa mpango wa upatikanaji wa ruzuku ya kutosha kwa kila mwanafunzi ungefikiwa. Hata hivyo, haoni iwapo mpango huo una manufaa kwa sasa kutokana na fedha kutotumwa shuleni inavyotakiwa.

“Pia zipo kampuni kubwa nyingi zinazoshirikiana na watendaji wa serikali kukwepa kulipa fedha ambazo zingewekezwa katika elimu, hiyo ina maana kwamba system yetu ya elimu itaendelea kuwa mbovu maana serikali haiwekezi. Lakini vilevile mahali ambapo fedha zinatoka zinaishiwa kuliwa na wajanja, “alisema.

wanafunzi-sambaru

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Sambaru, iliyopo wilaya ya Ikungi, mkoani Singida

Lissu alionya iwapo serikali itaendelea kuwakumbatia watendaji wezi, fedha za miradi ikiwemo ile ya elimu, taifa litabaki nyuma kielimu na kupitwa na nchi zingine za Afrika Mashariki ambazo zimepitia misukosuko ya aina mbalimbali.

Kwa mujibu wa MMEM, lengo la msingi la ruzuku kwa kila mwanafunzi ni kuziba pengo lililotokana na kuondolewa kwa ada kwa wanafunzi, ambapo inalenga kuinua ubora wa elimu kwa kuhakikisha kuwa rasilimali muhimu za kujifunzia zinapatikana shuleni. Katika bajeti ya mwaka 2009/2010, zaidi ya sh. bilioni 80 zilitengwa kwa ajili ya ruzuku.     

Kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali, asilimia 40 ya fedha za ruzuku zinazopelekwa shuleni katika MMEM hutumika kununulia vitabu, asilimia 20 hununulia vifaa vya kujifunzia, asilimia 20 hukarabati majengo na vifaa vya shule, asilimia 10 hugharimia mitihani na asilimia 10 hutumika kwa mambo ya utawala.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *