Giza nene mauaji ya RPC Mwanza, mwanamke aliyekuwa naye matatani

Sitta Tumma

UTATA mkubwa umegubika mauaji ya Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza (RPC), Liberatus Barlow ikiwa ni pamoja na utambulisho wa mwanamke aliyekuwa na marehemu kabla na wakati wa tukio hilo na mazingira ya tukio husika.

Marehemu Barlow aliuwawa na kundi la  watu wanaosadikika kuwa ni  majambazi waliommiminia risasi za moto sehemu mbali mbali za mwili wake, kisha kupoteza maisha papo hapo. Tukio hilo limetokea kati ya saa 7 na saa 8 usiku wa kuamkia leo, katika maeneo ya Kitangiri karibu na TAI FIVE hoteli barabara ya Kona ya Bwiru jijini Mwanza.

liberatus barlow enzi za uhai wake

Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Mwanza, Lily Matola, mauaji hayo ya kinyama dhidi ya Kamanda Barlow yalitekelezwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, na kwamba walifyatulia risasi maeneo ya shingoni.

Alisema, ingawa bado hawajafahamu idadi hasa ya risasi zilizosababisha kifo cha RPC huyo, tayari jeshi la polisi limeshaanza kufanya uchunguzi wake mkali na wa kitaalamu zaidi ili kuwakamata watu wote waliohusika katika shambulizi hilo la kinyama.

Taarifa za kutatanisha zimeelezwa kwamba, kabla RPC huyo hajafikwa na mauti alikwenda kushiriki kikao cha harusi ya mtoto wa dada yake aliyetajwa kwa jina la Sembeli Mareto, kilichofanyika Florida hoteli iliyopo maeneo ya Kitangiri, na kwamba kikao hicho cha harusi kilimalizika majira kati ya saa  4-6 usiku.

"Ni kweli Kamanda wetu wa Polisi Liberatus Barlow amefariki dunia kwa kupigwa risasi za moto. Ni tukio kubwa sana na la kinyama!. Haijafahamika alimiminiwa risasi ngapi hadi kufariki dunia papo hapo.

"Tayari upelelezi wa kina umeshaanza. Na tutahakikisha watu wote waliohusika katika shambulizi hilo wanakamatwa," alisema.

Taarifa zilieleza kwamba Kamanda Barlow alipingwa risasi sehemu za begani na kutokezea upande wa pili wa shingo akiwa kwenye gari lake binafsi Toyota pick up double cabin.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, Injinia Evarist Welle Ndikilo, aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake kwamba, mauaji hayo dhidi ya kiongozi huyo wa jeshi la polisi mkoani Mwanza, kamwe hayafumiliki.

Kwa mujibu wa RC Ndikilo, mara baada ya kikao hicho cha harusi kumalizika, Kamanda Barlo aliwasha gari lake kisha kurudi nyumbani, na wakati akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake alikutana na mwanamke mmoja njiani aliyetajwa kwa jina la Doroth Moses ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Nyamagana, mkazi wa Kitangili na alimpatia lifti kisha kumepeka hadi nyumbani kwake kwa usalama zaidi.

Alisema, wakati mwanamke huyo akijiandaa kuteremka kwenye gari la marehemu Barlow aingie nyumbani kwake, walitokea watu wawili wakiwa wamevalia sare za Polisi Jamii huku wakilimulika kwa tochi gari, na kwamba baada ya kuona hali hiyo, mwanamke huyo Doroth alimuuliza marehemu iwapo anawafahamu watu hao.

“Baada ya mwanamke huyo kumuuliza RPC kama anawafahamu watu hao, marehemu alisema anaona kama ni walinzi wa Jamii. Wakiwa bado wanaulizana wale watu walizidi kusogelea gari huku wakisema kwa nini mnatuwashia mwanga mkali na gari lenu?.

"Wakati watu hao wakiuliza hivyo huku wakiwa wanasogelea gari la RPC, marehemu Kamanda Barlow aliwauliza mimi hamnijui?. Wakati mama huyo anateremka kutoka kwenye gari, watu wengine kama watatu walisogelea lile gari, na ndipo marehemu alipochukua radio call yake ili kuwasiliana na askari wake”, alisema Ndikilo na kuongeza:

“Wakati anashika redio yake ili kuwasiliana, idadi ya watu kama watano hivi waliokuwa wamefika eneo hilo wakampiga risasi moja ya begani na kutokezea sehemu za shingoni. Baada ya shambulio hilo Kamanda wetu akawa amepoteza maisha papo hapo, wala hakuweza kupambana na wahalifu hao. Damu nyingi zilimwagika na watu hao wakakimbia na redio call hiyo pamoja na simu mbili za marehemu na pochi ya mama huyo iliyokuwa na kiasi cha pesa. "

Alisema kuwa hadi sasa mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi, na kuongeza kuwa jeshi la polisi makao makuu Dar es salaam limemtuma DCI Manumba kuongeza ulinzi na upelelezi wa kina katika tukio hilo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza, aliiitaka jamii na wakazi wa Mwanza kuwa na subila katika kipindi hiki cha majonzi katika kutafuta wahusika wa tukio hilo kwa uchunguzi unaoendelea wa vyombo vya dola.

Tetesi zinaeleza kwamba, tukio la kuuawa kwa Kamanda huyo huenda limesababishwa na uhasama na watu mbali mbali katika maeneo ya kazi alikowahi kufanyia, na kwamba hilo ni tukio linalotia shaka iwapo kama imetokea kwa bahati mbaya.

Baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na mahusiano ya kimapenzi, misimamo yake mikali ya kupambana na majambazi, ambapo alikuwa akitoa onyo kwa majambazi kutoingia katika eneo lake la kazi.

Kwa upande wao, watoto wa Doroth Moses walisema kwamba siku ya tukio mama yao aliwaaga jioni kuwa anakwenda katika kikao cha harusi cha rafiki yake, na wakati anarudi nyumbani  majira ya saa 4 usiku aliwapigia simu ili wamfungulie geti, na kwamba wakati mtoto mmoja Keny Rogers (17), akienda  kumfungulia geti aliona kundi la watu kama watano wakiwa wamezunguka gari.

"Yule mwanaume (RPC), aliyekuwa amemleta mama (Doroth), sisi hapa hatumjui na hata hatujawai kumuoana.  Lakini mama alitupigia simu akisema tumfungulie geti..

"Wakati mimi nimeenda kufungulia geti, niliona kundi la watu watano lakini mimi hawakunioana. Wakati naendelea kuwacheki (kuwaangalia), kama nawafahamu ama lah, ghafla nikasikia mlio wa bunduki kisha wale watu wakakimbia. Nikaanza kuona damu nyingi zinamwagika chini”, alisema mtoto Keny.

Awali iliripotiwa kwamba Doroth alikuwa ni dada wa marehemu Barlow.

Hili ni miongoni mwa matukio makubwa  ambayo yameripotiwa kutokea jijini Mwanza, ambapo hivi karibuni iliarifiwa kwamba, Ofisa mmoja wa Uhamiaji Mkoani Mwanza, Albert Buchafwe alinisurika kuuawa kwa risasi na mtu anayedaiwa kuwa ni Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Nyakato Mwatex (OCS), Abubakar Zebo baada ya kushukiwa kuwa ni jambazi. Ilidaiwa kwamba, Ofisa huyo wa Uhamiaji alifyatuliwa risasi tano wakati akijaribu kukimbia, na kwamba gari lake liliumizwa vibaya na risasi zilizokuwa zikifyatuliwa na OCS Abubakar, na kwamba tukio hilo lilithibitishwa na Ofisa huyo wa Uhamiaji pamoja na marehemu RPC Barlow.

Tukio jingine lilitokea miezi michache iliyopita, ni lile la mwanasiasa maarufu jijini hapa, Seni Manumbu aliyeuawa kwa kupigwa risasi za moto na watu wasiojulikana, wakati alipokuwa akifunguliwa geti ili aingie nyumbani kwake.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.

9 Comments
  • Hali ya mwanza mbona ni kama inatisha kwa hapo ilipofikia?

    inanisikitisha ni kwa kiasi gani watu wamekuwa wanyama kiasi hiki.

    lakini mwisho wa siku nadhani kwa mwenendo huu kuna haja ya kuangalia sera na taratibu za kumiliki silaha za moto, hii inatakiwa kufuatana na zoezi la uchunguzi wa mara kwa mara wa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, ni kweli itakuwa ni kazi ngumu sana kwa vyombo vya dola pekee kuifanya kazi hiyo ila nataka kuamini kuwa kama tutashirikiana watanzania wote kuwaripoti wale wote tunaoishinao mitaani na wanamiliki silaha bila kujali kama ni kwa halali ama haramu ili kuiachia dola kuamua ni yupi anamiliki kihalali kuliko kujua na kunyamaza tukiamini kuwa huenda inamilikiwa kihalali maana imeshakuwa ngumu kuweza kutambua ni nani anamiliki kihalali na ni nani si halali.

    POLENI SANA FAMILIA YA MAREHEMU L.BARLOW, WAKAZI WA MWANZA NA WATANZANIA KWA UJUMLA.

    MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU SALAMA

  • Jamani watanzania tuweni na huruma,jeshi letu la police mbona hamuwapi makamanda ulinzi wa kati wote

    • Ndugu yangu naungana na wewe katika majonzi ya Kamanda Barlow, Watanzania tumefikia hatua hii kweli?.Alikuwa kiungo muhimu sana katika kutekeleza matakwa ya mfumo wetu mzuri,wana wa Mwanza wanamwelewa sana na wamepata pigo kubwa sana kwa kumpoteza.Kila la kheri kwa tume ya uchunguzi.MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI.

  • poleni sana familia ya marehemu kamanda Barow na natumaini jeshi la polosi litafanya kazi yake ili kubaini waalifu wote ili watanzania waishi kwa amani bila woga wa mali na maisha yao.

    • Ndugu yangu nawe,mmmh,unauliza kwanini mauaji mengine hatumwiti Manumba Robert,kama yapi,kwenye migodi?,maandamano ya vyama vya upinzani?,Wavamizi (wazawa) wa Wawindaji wa kigeni?,Wavuvi wadogo wadogo ziwani dhidi ya wawekezaji wa kigeni?,kuchomwa kwa makanisa?.Acha sie tufe tu.Lakini kiongozi wetu hapana,haiwezekani kabisa. Tume chunguza kamata wote tia ndani.

  • Ndg, watanzania wote wenye na wasio na mapenzi mema na nchi yetu hapo ndipo tulipo leo ebu tujiulize kesho tutakuwa wapi?Ninachoweza kusema leo kutokana na tukio hili kuwasihi wanadamu kumrudia MUNGU kuwa na hofu ya MUNGU.Tuwe watu wa msamaha tusiwe watu wa visasi.

  • Kama haki ikitendeka sawasawa yatajiri mengi ambayo yamejificha ndani ya sakata hili, tatizo ni hawa watu wetu wanaochungza hili jambo kama watakuwa tayari kusema ukweli, na ukweli mtupu. Tume inayojitegemea ni muhimu ili kujiepusha na hili, ije na mawazo ya jinsi ya kuliepuka janga kama hili siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *