KWA takribani miaka mia mbili na zaidi dunia imetawaliwa na mfumo mmoja wa kuleta maendeleo ukiasisiwa kwa mawazo na shinikizo kutoka kwenye nchi za Magharibi na Marekani.
Nchi za Magharibi na Marekani zinaendelea kushinikiza nchi zote duniani kukubali mfumo wa maendeleo kama wanavyoona wao inafaa na huku wakilazimisha nchi zingine ziwe kama wao. Mabepari hawa wanataka kila nchi iige mfumo wao wa ubepari wa binafsi (Private Capitalism), demokrasia (Liberal Democracy) na kipaumbele kwa haki za kisiasa juu ya haki za uchumi (Emphasis on political rights over economic rights).
Swali linakuja je, nchi za Magharibi na Marekani ziliendelea kwa kuwa na demokrasia?
Tukirejea katika historia tutagundua ya kuwa maendeleo yaliyoanza kuonekana kwenye mapinduzi ya viwanda kwenye nchi za Ulaya na baadae kule Marekani hayakuletwa na demokrasia. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba maendeleo yalikuja kwanza ndio demokrasia ikafuata.
Mapinduzi ya viwanda yalianza kuanzia miaka ya 1760 kuelekea 1820 na kushika kasi ya hali ya juu kuanzia mwaka 1840. Kwa muda wote huu wa mapinduzi ya viwanda hakuna nchi yoyote ya Ulaya ama Marekani ilikuwa na demokrasia na si kweli kwamba demokrasia ilileta maendeleo bali ni maendeleo yaliyoleta demokrasia.
Kwa kudhihirisha hili, demokrasia ilianza kujitokeza nchini Uingereza kuanzia mwaka 1850 baada ya mapinduzi ya viwanda ambako ni asilimia mbili tu ya wanaume ndo walikuwa wanaruhusiwa kupiga kura. Na kuanzia mwaka 1880 asilimia kubwa ya wanaume ndio waliruhusiwa kupiga kura na sio wanawake.
Kwa Marekani hali haikuwa tofauti sana kwani kuanzia mwaka 1860 baada ya mapinduzi wa viwanda wazungu wengi wa kiume ndio waliruhusiwa kupiga kura. Wanawake wa kizungu waliruhusiwa kupiga kura kuanzia mwaka 1920 ili hali watu weusi waliruhusiwa kupiga kura kuanzia mwaka 1960.
Hii inatupa tasfiri gani? Nchi za Magharibi na Marekani kipaumbele chao hakikuwa demokrasia bali ilikuwa kukuza uchumi wa nchi zao kwanza ili kuwa na taifa imara kabla ya kuwa na demokrasia.
Hebu tugeukie Afrika na kuona hali ikoje, Afrika ambapo nchi nyingi katika bara hili ni changa zimelazimishwa kuanza na kutafuta demokrasia kabla ya uchumi imara. Mashinikizo mengi kutoka Benki ya Dunia na IMF yanalazimisha nchi kufuata mifumo ya demokrasia kama waliyoianisha ili kutoa mikopo na misaada na kinyume chake nchi ikikaidi misaada na mikopo husitishwa.
Tafiti zimeenda mbali na kudhihirisha ya kuwa ili kuwe na demokrasia imara yenye kuleta tija kwa watu wake ni lazima kuwe na uchumi imara kwa watu ila kinyume cha hapo demokrasia inakosa maana yake. Tafiti hizi zinadhirisha ya kwamba, kama pato la mtu mmoja mmoja (per capital income) kwa mwaka ni dola elfu moja za Marekani kutakuwa na demokrasia kwa miaka 8.5, na kama pato la mtu mmoja mmoja ni kati ya dola elfu mbili na elfu nne kwa mwaka kutakuwa na demokrasia ya miaka 33, na kama pato la mtu mmoja mmoja ni kati ya dola elfu sita na kwenda mbele kwa mwaka kutakuwa na demokrasia milele. Soma kitabu cha mchumi nguli Dambisa Moyo HOW THE WEST WAS LOST.
Tafsiri ya utafiti huu inatuambia nini? Ongezeko la uchumi wa kati kwa wananchi ndio nguzo muhimu katika demokrasia na ndio wanaoweza kuiwajibisha serikali lakini wananchi wakiwa masikini hawana uwezo wa kuiwajibisha serikali yao kikamilifu. Natumaini sisi sote ni mashuhuda wa hili tukiitafakari Tanzania yetu.
Ukienda mbali na kujiuliza zaidi, nchi zinazojitapa kuwa na demokrasia je, ni kweli demokrasia hiyo ipo kikamilifu ama ni ishara za uwepo kwa demokrasia tu?
Tafiti zilizofanywa na Freedom House mwaka 2013 katika nchi 196 zinaonyesha ya kuwa asilimia 50 ya nchi hizo hazina demokrasia ya kweli (Illiberal democracies) kwa maana ya kwamba watu hawana uhuru wa kujieleza na hawaruhusiwi kutembea vile watakavyo. Tafiti hizi zimeenda mbali na kusema ya kuwa, tangu mwaka 2006 mpaka 2013 demokrasia na uhuru vimekuwa vikiporomoka kwa kasi ya ajabu kila mwaka.
Tukirejea katika historia tutakumbuka ya kuwa China katika miaka ya 1820 ilikuwa nchi yenye uchumi imara kuliko zote duniani ilihali haikuwa na demokrasia na mpaka leo tunashuhudia China ikirudi kwa kasi kama nchi ya pili duniani yenye uchumi imara bila kuwa na demokrasia. China inatuonyesha sio lazima kuwa na domokrasia ili kupata uchumi imara bali ni uchumi imara ndo huleta demokrasia imara.
Mantiki ya makala yangu leo hii sio kuonyesha ya kuwa demokrasia ni mbaya la hasha! Ila ni kujaribu kutafakari kwa kina na kujiuliza maswali magumu je, ni lazima kila nchi duniani ifuate nchi za Magharibi na Marekani kwa kuwa na demokrasia sawa sawa na ile waitakayo wao?
Ukweli ni kwamba, hakuna mfumo mmoja unaoweza kuiongoza kila nchi duniani kama vile watakavyo mabepari hawa, ila kunaweza kuwe na mifumo mingi ya kufanya kuwe na maendeleo kama vile China inavyotuonyesha leo hii ama vile Japan wenye demokrasia ila ni tofauti sana na ile ambayo nchi za Magharibi na Marekani zinahubiri.
Demokrasia kwa Afrika inashindwa kuzaa matunda kama vile mabwana wakubwa wanavyotaka kwa kuwa sio kitu ambacho siye tunaamini bali tunafanya kwa kuwa tumeshurutishwa. Hebu tafakari kwa muda kidogo na jiulize je, ni nchi gani Afrika inaweza kujivunia ya kuwa inademokrasia ya kweli? Ama demokrasia tunayoizungumzia ni kuchagua viongozi wetu kila baada ya miaka mitano tu baada ya hapo ndo mwisho wa demokrasia?
Kama Afrika inataka kuona maendeleo imara kama vile tunavyohitaji ni dhahiri inatupasa kuwa na demokrasia inayotokana na Waafrika wenyewe na sio hiyo tunayoinunua huko ughaibuni ambapo badala ya demokrasia kutuletea maendeleo ndo inazidi kutudidimiza kwa kuleta vita za wenyewe kwa wenyewe ama kuminya uhuru wa watu kwa kiasi kikubwa ili kundi fulani la wachache lifaidike.
Kwa kuhitimisha, ni dhahiri sasa demokrasia imedhihirika sio sehemu muhimu ya kuleta maendeleo ila demokrasia ni matokeo ya kuwa na uchumi imara. Mara nyingi imekuwa ikijidhihirsha ya kuwa nchi za Marekani na Magharibi zimekuwa zikitaka Afrika iwe kama wao kwa kuwa na maendeleo na kufuata demokrasia ila kama kweli wanataka tuwe kama wao ni lazima tupate uchumi imara kwanza ndo demokrasia baadae kama walivyofanya wao na sio kama vile tunavyofanya sasa.