‘Kwa nini nachimba dhahabu mtoni?’

Kulwa Magwa

RAMADHAN Abdul (19) anaishi na wazazi wake katika kijiji ambacho ajira kubwa ni kilimo. Kijana huyo anaishi kijiji cha Kibangile, kilichoko katika kata ya Kisemu, tarafa ya Matombo, mkoani Morogoro.

Hata hivyo, maisha yake ya shule yalimalizika alipomaliza darasa la saba, miaka minne iliyopita, kijijini hapo, na tangu wakati huo hajawahi kuingia katika chumba kinachoitwa darasa kusomea taaluma yoyote.

Ingawa unapozungumza naye fikra alizo nazo ni kusoma, huku akitamani siku zirudi nyuma arejee darasani akasome. Anaamini kwamba iwapo atarudi darasani, huenda bahati ‘aliyochezea’ siku za nyuma itakuwa kweli; na atafanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Abdul anasema, baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari alijikita katika shughuli ya kilimo akisaidiana na wazazi wake, lakini kadri miaka inavyokwenda, upatikanaji wa mazao umekuwa ukishuka suala ambalo linawaumiza vichwa.

Kutokana na hali hiyo, miaka miwili iliyopita alianza kuchimba madini ya dhahabu kwenye mto Wami/Ruvu unaopita kijijini hapo.

Anasema, licha ya kwamba kazi hiyo anaifanya kutotakiwa kisheria, imekuwa ikimuwezesha kuendesha maisha ya familia yake – ambapo kipato anachopata ndicho anachonunulia chakula, mavazi na huduma za kifamilia.

Kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010, sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na sheria ya rasilimali za maji Na.11 ya mwaka 2009 zinapiga marufuku shughuli za uchimbaji au shughuli zozote za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, mtoni au ziwani.

Pia sheria ya rasilimali za maji inazuia shughuli zote za kibinadamu kufanyika ndani ya mita 60 kutoka mahali yalipo maji yanayotegemewa na watu kwa matumizi mbalimbali.

Abdul anasema kazi hiyo inampatia hadi sh. 7,000, suala linalomhamasisha kuendelea kuifanya, licha ya kwamba anajua anachofanya ni kinyume cha sheria.

“Siku nyingine siambulii kitu, maana madini yenyewe yako kwenye maji na maji muda wote yanasafiri,“anasema kijana huyo.

Anasema familia inayomtegemea imekuwa ikiongezeka kila mara kutokana na ndugu wanaowatembelea ambapo wengine huweka ‘makazi’, hivyo kumfanya kama kijana anayetegemewa na wazazi kuwa na jukumu kubwa kuhakikisha mambo ‘hayaribiki’ nyumbani.

Kijana huyo anasema, kabla ya kujikita kwenye uchimbaji wa dhahabu mtoni alikuwa mkulima wa mahindi na ufuta, ambapo mavuno aliyokuwa akipata yalimsaidia kununua mavazi. Hata hivyo, miaka mitatu iliyopita baba yake alipooza upande mmoja wa mwili, suala lililomfanya ajitishwe jukumu la kuhudumia familia yao.

Anasema, mwanzoni mwa mwaka juzi aliungana na wenzake kwa lengo kuchimba madini na tangu wakati huo wanachimba dhahabu kwa ‘siri’ katikati ya mto na pembezoni mwa kingo za mto huo.

wami-1

Kingo mojawapo ya mto Wami ambayo imeathiriwa na shughuli za uchimbaji madini, katika kijiji cha Kibangile, mkoani Morogoro

Ingawa nia ya kuacha kazi hiyo anayo, lakini anasema hajapata mtaji anaoutaka atakaoutumia kufanyia biashara.

“Nahangaika sana, lakini sipati hiyo hela (ya mtaji). Lengo langu nikipata kama sh. 400,000 naacha kabisa uchimbaji maana ni hatari kubwa ukikamatwa, “anasema.

Hata hivyo, Abdul anasisitiza hataacha kuchimba katika mto huo mpaka atakapowezeshwa au kupatiwa njia mbadala ya kuendeshea maisha ya familia yake, ingawa hataki kusikia kuhusu kilimo.

Anasema kilimo wanachofanya watu wengi sehemu hiyo hakitabiriki kutokana na mvua kutokuwa za uhakika.

Akizungumzia uchimbaji katika mto huo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, George Malecela, anasema wapo watu wengi wanaochimba kwa kificho licha ya kuwazuia kufanya hivyo.

“Juhudi za kuwaondoka zimekuwa zikigonga ukuta kutokana na Jeshi la Polisi kuwakamata na kisha kuwaachia, “anasema mtendaji huyo wa kijiji.

Anasema, vijana wanaochimba wengi wao wanafanya kwa kujificha, kufuatia amri iliyotolewa hivi karibuni na maofisa wa Ofisi ya Bonde la Maji la Mto Wami/Ruvu, waliofika sehemu hiyo.

“Hata hivyo, wapo hao wachache ambao hata sisi kama kijiji tunashindwa kuwakamata maana hututishia maisha. Kwa sasa tunasubiri vikao vinavyotarajiwa hivi karibuni vitoe amri ya kupiga marufuku na Polisi waagizwe kuja kulinda mto huu, “anasema Malecela.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Madini Mkazi wa mkoa wa Morogoro, Lucy Kimaro, anasema wamekuwa wakijitahidi kila mara kuwatimua wachimbaji hao, lakini wameshindwa kufanikiwa.

Lucy anasema, tatizo lililopo sehemu hiyo linatokana na baadhi ya wazazi kuwahamasisha watoto wao kuchimba madini mtoni suala ambalo ni kinyume cha sheria.

“Pia hao watu wanachimba bila leseni na hata wangekuwa nazo, hairuhusiwi kuchimba mtoni, hivyo tunajiandaa pamoja na wadau wengine tudhibiti kabisa tatizo hilo,“anasema.

Msimamizi wa Ofisi ya Bonde la Maji la Mto Wami/Ruvu kijijini hapo, Gilbert Ngahimila, anasema vyanzo vingi vya maji katika sehemu hiyo vimeathiriwa na shughuli za kibinadamu, ukiwemo uchimbaji wa dhahabu na kilimo jirani na mto.

Msimamizi-wami

Msimamizi wa Ofisi ya Bonde la Maji la Mto Wami, katika kijiji cha Kibangile, Gilbert Ngahimila, akionyesha uharibifu wa ardhi unaofanywa na wachimbaji madini kwenye mto huo

Anasema, iwapo mkakati wa kitaifa hautafanyika, mto huo ambao ni chanzo kikubwa cha maji kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, unaweza kutoweka miaka michache ijayo.

“Nguvu kubwa inatakiwa maana mto huu una mito mingi midogo inayoingia humu ambayo inaathiriwa na shughuli hizo, na bahati mbaya huu ni mto ni mrefu sana hivyo kudhibiti kila kinachofanywa inahitaji rasilimali kubwa ya fedha na watu, “anasema Ngahimila.

Kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji, malengo yaliyopo ni kuhakikisha rasilimali za maji nchini zinatunzwa, zinatumiwa, zinaendelezwa, zinaboreshwa, zinasimamiwa na kudhibitiwa kwa kuwa ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu kwa kizazi kilichopo na vijavyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *