Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema afya ya Tundu Lissu imeimarika na ataingia katika awamu ya tatu ya matibabu nje ya Nairobi.
Tundu Lissu alipelekwa jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu na kulazwa katika hospitali ya Nairobi baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana katika makazi yake mjini Dodoma mapema mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam katika Makao Makuu ya chama hicho, Mbowe amesema hali ya kiafya ya Mhe Lissu inaendelea vizuri ambapo ametoka katika kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) na anatarajiwa kuingia katika awamu ya tatu ya matibabu ambayo yatafanyika nje ya nchi.
“Kwa kadiri ya madaktari watakavyoshauri lakini kwa hali ya sasa, katika kipindi cha wiki moja Mhe. Lissu atamaliza awamu ya pili ya matibabu yake ya Nairobi na atasubiri kupelekwa katika awamu ya tatu ambayo itafanyika nje ya Nairobi”, amsema Mbowe.
Ameeleza kuwa siku chache zijazo Lissu ataondolewa katika hospitali ya Nairobi na kuingia awamu ya tatu ya matibabu ambayo itafanyika nje ya nchi na itachukua muda mrefu mpaka mgonjwa arejee katika hali yake ya kawaida.
“Katika hatua ya sasa hatutawaambia anakwenda wapi lakini itoshe tu kuwaambia kwamba ataanza awamu ya tatu na ya muda mrefu ya matibabu katika hatua inayoitwa ‘rehabilition’. Kwa hiyo atakapokwenda kutibiwa hilo litatangazwa kwa wakati mwafaka na katika kipindi kifupi Mhe. Lissu ataruhusiwa kutoka katika hospitali ya Nairobi”. Amefanunua Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe amesema katika awamu ya tatu ya matibabu ya Lissu, CHADEMA hawatakuwa wasemaji wa mgonjwa lakini jukumu hilo wanaiachia familia ya Lisu ambao watawajibika kutoa taarifa za Lisu kama watakavyopenda.
“Baada ya matibabu ya Nairobi, familia imeimarika na mgonjwa anajitambua vizuri ni lazima tuwaachie nafasi ya kufanya maamuzi ya ndani sisi (CHADEMA) tutakuwa nyuma na jukumu la usemaji tutalikabidhi rasmi kwa familia. Tutasaidia pale tutakapohitajika kusaidia” amesema Mbowe.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiongea na wanahabari
Kwa mujibu wa Mbowe ameeleza kuwa matibabu ya Lissu nchini Kenya mpaka kufikia tarehe 12 Oktoba mwaka huu yametumia zaidi ya milioni 240 kuokoa uhai wake. Gharama zote za matibabu na kuwalipa madaktari tangu Lissu aanze kutibiwa zimetumika zaidi milioni 412.7 ambazo zimechangwa na wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, wafanyabiashara pamoja na wananchi wengine.
Alipoulizwa kuhusu dereva wa Lissu ambaye yuko nchini Kenya na ambaye amekuwa akihitajika na Jeshi la Polisi katika upelelezi wa tukio la kupigwa risasi kwa Lissu, Mbowe amesema dereva huyo bado anaendelea na matibabu ya Kisaikolojia na kama Polisi wanamuhitaji wakamchukue kwasababu jukumu la kumkamata sio lao.
Taarifa hiyo ya CHADEMA kwa vyombo vya habari inakuja wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upepelezi na mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. Baadhi ya wananchi walishauri waitwe wapelelezi kutoka nje (Scotland Yard) au iundwe tume huru ili kuchunguza tukio na kupata ukweli wa nani anahusika na udhalimu huo.
Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulika mnamo Septemba 7 mwaka huu muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Bunge. Tukio hilo lilitokea katika makazi yake mjini Dodoma ambapo inaelezwa kuwa wakati akitoka bungeni alikuwa akifuatiliwa na gari mpaka alipofika nyumbani ndipo waharifu hao walianza kurusha risasi mfululizo kwenye gari ambalo Lissu alikuwamo ndani na dereva wake.
Risasi kadhaa zilimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili na baada ya muda mfupi alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Dodoma. Huko alipata matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Nairobi nchini Kenya ambako ameendelea kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa.
Mpaka kufikia sasa ametimiza mwezi mmoja. Taarifa zinaeleza kuwa hali yake imeimarika na ameenza kula na kuongea. Kutokana na makubaliano ya familia yake na madaktari anatarajiwa kusafirishwa nje ya Kenya kwa hatua ya tatu ya matibabu ili kumsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida.