Mahabusu yenye umri wa miaka 68

Kulwa Magwa

UNAPOFIKA kwenye ofisi ya kijiji cha Mwadui-Lohumbo, kilichopo mashariki mwa mji mdogo wa Maganzo, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, utakutana na  majengo yenye yaliyojengwa enzi za ukoloni wa Waingereza.

Majengo hayo ni pamoja na mahakama, ofisi ya kijiji, nyumba ya mtendaji wa kijiji  na madarasa mawili ya shule ya msingi ya Mwadui DDC, ambapo yote yalijengwa miaka 68 iliyopita.

Kinachofurahisha kwa majengo hayo ambayo wenyeji wanasema yalijengwa na uongozi wa mwanzo wa kampuni ya Williamson Diamonds inayochimba almasi, sehemu hiyo, ni kuwa bado yako imara licha ya kwamba katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya kuta zimeanza kupata nyufa.

Kutokana na historia yaliyobeba, majengo hayo yanavutia kwa shughuli za utalii na hasa unaposikiliza wenyeji wakiyazungumzia, kiasi kwamba iwapo yangekuwa mijini, basi ‘mvuto’ huo wa maelezo ungevutia wengi kuyatembelea.

Mathalan, wenyeji wanasema jengo la mahakama ndilo lililotoa jina la awali la kijiji hicho ambacho kilifahamika kwa jila la ‘Utemini’ kabla ya kubadilishwa miaka michache iliyopita na kuitwa Mwadui-Lohumbo.

Wanasema, neno ‘utemini’ ambalo kwa lugha ya wenyeji Wasukuma linamaanisha ufalme, lilitokana na watu kutoka sehemu mbalimbali waliokuwa wakitafuta haki kuelekezwa kuwa wangeipata katika jengo hilo la mahakama.

Joseph Jisena (52), ambaye pia ni mwenyekiti wa kijiji hicho, anasema umaarufu uliotokana na jina hilo ulisaidia kukifanya kijiji chao kifahamike hadi nje ya mkoa wa Shinyanga, suala ambalo liliwaweka kwenye ‘ramani’ enzi hizo.

“Ndiyo maana hapa (kijijini) hata baada ya kufutwa kwa jina hilo pamebaki kuwa maarufu kama Utemini,“anasema Jisena.

Hata hivyo, licha ya jengo hilo kuwa na ofisi na mahabusu, mahakama ilihamishwa kijijini hapo na kupelekwa Maganzo, kutokana na kile kinachoelezwa na wenyeji kwamba waliokuwa watumishi walichoshwa na maisha ya kijijini.

mahabusu

Chumba cha Mahabusu ya kijiji cha Mwadui – Lohumbo

Wanasema, watumishi hao walihama na makabrasha yao, lakini hata mahakama wanayoendesha huko Maganzo imebaki kuitwa jina la Mahakama ya Mwanzo Mwadui-Lohumbo.

Nyuma ya jengo hilo la mahakama – kwa ndani – kuna jengo dogo ambalo tangu enzi za ukoloni limekuwa likitumika kama mahabusu ya watu wanaokamatwa kijijini hapo kwa tuhuma mbalimbali, ambao huhifadhiwa humo kabla ya kupelekwa mahakamani, Maganzo.

Jengo hilo lina urefu wa futi nne (kwenda juu) na upana usiozidi futi 12 na mtuhumiwa anapokamatwa iwapo ni mrefu zaidi ya futi nne, hulazimika kuinama aingizwapo ndani na pia awapo ndani hawezi kusimama.

Jisena anasema, licha ya kwamba mahakama imehama sehemu hiyo wameendelea kuitumia mahabusu hiyo kuhifadhi wahalifu wao kwa kuwa hawana sehemu nyingine wanayoweza kuwatunza.

“Tunajua kwamba kuna suala la haki za binadamu, lakini hatuna uwezo wa kujenga mahabusu nyingine kwa ajili ya kuwaweka watu hao ndiyo maana tunaitumia hii,“ anasema mwenyekiti huyo.

Anasema, licha ya kwamba wamekuwa wakitumia mahabusu hiyo ya aina yake,  mara nyingi wahalifu hutoroka kutokana na kutokuwepo kwa mlinzi wa kuwalinda. Hiyo ndiyo mahabusu iliyoko katika jengo la mahakama lililojengwa mwaka 1945.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *