Mapungufu ya Huduma Bora ya Afya Vijijini

Belinda Habibu

Kilio cha upungufu wa vifaa tiba, wataalamu hawatoshi na miundombinu ya baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati kuwa mibovu ni moja ya sababu ya ongezeko la vifo vya kinamama wajawazito wakati wa kujifungua.

Zahanati ya kijiji cha Magalata, wilaya ya Kishapu, mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa nyingi nchini ambazo hukosa mashine za kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa muda mrefu, huku ikiwa na wafanyakazi wawili ambao ni wauguzi, haina dawa za kutosha wala nyumba za watumishi.

Muuguzi wa zahanati hiyo, Zuhura Suleimani, aliyekuwepo hapo tangu mwaka 1997, alisema kuna wakati wanawazalisha kinamama bila kufahamu hali zao za afya kwa kuwa vitendanishi vya VVU hukosekana.

“Mazingira ya kazi yana changamoto nyingi, hatuna mashine ya kupima hata malaria, tunasikiliza historia ya mgonjwa na kumhudumia,”alisema muuguzi huyo.

Alisema toka mwaka 2006 zahanati hiyo haina daktari baada ya aliyekuwepo kwenda kusoma na hakurudi, suala ambalo linawafanya wauguzi hao kufanya kazi kama madaktari na wakati huohuo wakiwa ndio wauguzi.

“Kama sasa mwenzangu yuko likizo na amekwenda semina pia, nimebaki peke yangu, wakija kinamama wawili tu kwa mfano wanahitaji kuzalishwa sijui kitatokea nini kwa mwanamke mmoja ambaye sitaweza kumhudumia kwa wakati,”alisema Zuhura.

Alisema mahali anakoishi ni kilometa moja kutoka zahanati hiyo ilipo, ambapo suala la usafiri kwake pia ni changamoto kwa kuwa anapokuwa nyumbani na mgonjwa au mjamzito akiletwa, huwa hekaheka ya kumkimbilia.

Zuhura aliongeza kuwa kadi za kinamama pindi wanapokuwa wajawazito na mahitaji ya kujaziwa hali ya maendeleo ya mimba, huwa zinakosekana kwa kipindi kirefu na kulazimu kutumia daftari.

“Kama wamekuja wanne itabidi wasubiri tu mpaka nimalize kuchora katika daftari kama kadi halisi zilivyo katika daftari zao, hunichukua hata saa nne na zaidi kumaliza,”alisema muuguzi huyo.

Alisema kinamama wengi hujifungulia nyumbani hasa wale wenye vidokezo vya hatari ambao huwaambia waende hospitali kuu, kwa sababu ya gharama na umbali wa zaidi ya kilometa 80 kufika, hivyo huamua kuzalia nyumbani. Kutoka Magalata hadi Kishapu mjini ni zaidi ya kilometa 80.

Zuhura alisema dawa za kukata damu zinazoshauriwa kuwepo katika zahanati pindi mjamzito anapojifungua, hukosekana mara kwa mara kwa kipindi kirefu na hiyo ni hatari.

Pamoja na jitihada mbalimbali wanazofanya wauguzi hao kunusuru maisha ya wajawazito na wagonjwa wengine, pia hulazimika kufanya usafi wa mazingira ya zahanati, kufyeka na kufua mashuka ya wagonjwa na kuwatibu wale wanaoumwa malaria, kushona vidonda, kuhara, kliniki ya kinamama na kuzalisha, kutoa chanjo kwa watoto na magonjwa mengine.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bulugu Mipawa, alisema kutokana miundombinu mibovu ya barabara hakuna basi linalokwenda katika vijiji vilivyoko sehemu hiyo.

“Hakuna madaraja ya uhakika kipindi cha mvua, ukipanda pikipiki (bodaboda) hadi Mhunze ni sh. 50,000 na kufika Shinyanga mjini kwa gari la kukodi ni sh. 250,000,” alisema Mipawa.

Dk. Moke Magoma wa Evidence for Action, anasema katika hatua zote za mtoto kuletwa duniani, lazima kila upande uwajibike kwa kuwa mimba siyo ugonjwa na kusisitiza kuwa maandalizi ni muhimu yafanyika mapema.

“Kwa upande wa familia lazima wajiandae kumpokea mtoto anayekuja kwa kuhakikisha mama anakula vizuri, anapumzika na kuwahishwa sehemu ya kutolea huduma ya afya mapema – iwe hospitali, kituo cha afya ama zahanati,”anasema Dk. Magoma.

Anaongeza kuwa mjamzito anapofika hospitali, kituo cha afya au zahanati anapaswa akute mahitaji yote yapo. Mahitaji hayo ni dawa, wahudumu wa afya waliohitimu mafunzo vizuri na damu salama.

Zahanati ya Mwadui-Lohumbo, iliyopo katika wilaya hiyo, haina tofauti kubwa na ile ya Magalata katika suala la huduma, vitendea kazi na wahudumu. Zahanati hiyo ina muuguzi mmoja na daktari mmoja.

Mkunga mstaafu wa zahanati hiyo, Elizabeth Bushesha, alisema mazingira ya kazi ya sasa na ya zamani katika kutoa huduma yako tofauti.

“Enzi zetu dawa zilikuwepo na mazingira ya kazi kwa ujumla yalikuwa mazuri, hapa pana nyumba ya wauguzi ukweli ni gofu,”alisema Elizabeth aliyefanya kazi katika zahanati hiyo kati ya mwaka 1980 hadi 1997.

Alisema kijijini hapo wapo wakunga wawili wastaafu, lakini kutokana na kutokuwepo kwa wahudumu wa afya wa kutosha, wamekuwa wakijitolea kuzalisha wajawazito.

“Hatulipwi na serikali kama ukitoa huduma hiyo kwa mama, basi ndugu zake au mumewe wakiamua kukupa asante basi unashukuru,”alisema mkunga huyo.

Alisema kinamama wanaoishi mbali hupelekwa katika zahanati hiyo kwa pikipii au baiskeli na kama kuna dharura, wakunga hao humfuata mjamzito anakokuwa kwa kusaidiana na ndugu zake.

Wauguzi hao wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa tiba – kama mashine ya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi na wakati mwingine mipira ya kuvaa mikononi (gloves), suala ambalo ni hatari kwao na wajawazito na motto anayezaliwa.

Muuguzi huyo anatoa wito kwa serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, hasa vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watu, ikizingatiwa kwamba hospitali kubwa ziko mbali na hakuna usafiri wa kuzifikia kwa urahisi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Makelele, alisema zahanati ya Mwadui Lohumbo haina mashine ya kupima virusi vya ukimwi, ingawa awali ilikuwepo na iliharibika, ambapo tangu wakati huo haijawahi kupelekwa nyingine.

“Mashine ya sasa ina gharama na zinakuja chache, tunaagiza (kutoka Bohari ya Dawa nchini-MSD) 100, tunaletewa 40 kinachofuata zahanati nyingi zinakosa,”alisema mganga huyo.

Kutokuwepo kwa mashine hizo kunaweza kuongeza idadi ya watoto wenye virusi vya ukimwi na kwamba, iwapo zinatumiwa wakati wa kujifungu husaidia kuwakinga na maambukizi.

Akizungumzia upungufu wa vifaa tiba kwa ujumla, Mganga Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Dk. Mwendo Msengi, alisema katika hospitali ya wilaya hiyo, mwaka jana, madaktari wanne waliacha kazi kwa sababu waliona hawafanyi kazi waliyoisomea kutokana na uhaba wa dawa na vifaa vya kazi.

Pamoja na changamoto za tiba, vifaa tiba na wataalamu wa afya, zahanati ya Mwadui-Lohumbo inakabiliwa na tatizo la vyoo kujaa na kuchakaa, huku vikiwa vimezungukwa na nyasi ndefu.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Musiba Athanas, anasema hana taarifa ya zahanati hiyo kuwa vyoo vyake havifai kwa matumizi .

Kaimu Ofisa Afya wa wilaya hiyo, Daniel Madaha, anasema wameweka mkakati kati ya wananchi na wahudumu wa afya kupitia kamati za afya za vijijini, ili kuhakikisha kuwa mazingira ya zahanati na vituo vya afya yanakuwa safi muda wote.

“Wananchi kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (NHIF) wanachanga fedha nyingi na matumizi yake ni pamoja na ukarabati mdogo mdogo kama wa vyoo, kununua dawa na vifaa,”alisema Madaha.

Aliongeza kwamba, sheria ya afya ya mwaka 2009, inasema kama hali ya mazingira ya zahanati, kituo na hospitali siyo nzuri, idara ya afya wilaya inampa mamlaka ya kuifunga, baada ya kutoa notisi ya siku 14.

“Tumeshafunga zahanati tatu mwaka jana (2012) mwezi wa tisa kwa sababu ya kutokuwa na vyoo, nazo ni zahanati ya Hilebelebe, Kinampanda na Beledi ambazo tulizifunga kwa wiki mbili na ndani ya siku 10 walijenga vyoo,”alisema ofisa huyo.

Kuhusu upungufu wa wahudumu wa afya katika zahanati hizo, kaimu mganga mkuu alisema tatizo hilo linashabihiana na zahanati za Nyenze, Bulima, Ngeme, Ikonda, Seseko, Kisesa, Mwajidalala na Beledi ambazo zinaongozwa na mhudumu wa afya mmoja mmoja aliyepewa mafunzo.

“Suala la upungufu wa watumishi wa afya ni janga la kitaifa na wilaya ya Kishapu imeathirika sana,”aliongeza mganga huyo.

Uchunguzi unaonyesha kwamba hospitali, vituo vya afya na zahanati za mijini, wafanyakazi wa afya wana zamu za kuingia kazini tofauti na vijijini ambako ni wachache.

Hali iliyopo katika zahanati hizo mbili iliwahi kuripotiwa katika katika zahanati ya Ifinga, mkoani Ruvuma na ile ya Kiegei, wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi ambazo zinakabiliwa na uhaba wa watalaamu wa afya pamoja vifaa tiba.

Katika kituo cha afya cha Kinesi, wilaya ya Rorya, hakuna shimo la kutupa kondo la nyuma la baada ya mjamzito kujifungua ambapo mama aliyejifungua hukabidhiwa na kutakiwa kuondoka nalo, huku kukiwa na changamoto ya wagonjwa wa maradhi mbalimbali kulazwa pamoja na wajawazito kwenye wodi mbili zilizopo sehemu hiyo.

Aidha, kwenye kituo cha afya cha Iguna, hakuna ‘gloves’, huku kukiwa na vitanda 12 ambapo mahitaji ni zaidi ya 20 na hakuna mashine ya kupimia damu.

Changamoto za afya pia zipo katika Hospitali ya Butiama, ambayo haina mifuko ya kuhifadhia damu inayotumiwa kumuongezea mgonjwa au mjamzito na kwamba iwapo mgonjwa anakuwa na tatizo la damu, inabidi ndugu au jamaa zake wakanunue katika maduka ya dawa ndipo awekewe.

Utafiti uliofanywa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Sikika na kuchapishwa katika jarida lake la Septemba 3, mwaka juzi, unaonyesha katika wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, kuna tatizo kubwa la makazi kwa wahudumu wa afya, ambao hulazimika kuishi katika vibanda vya nyasi.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyofuatiwa na ile ya mwaka 2007, msisitizo wake ulikuwa
kuinua hali ya afya za wananchi na kipaumbele kitolewe kwa makundi yaliyo hatarini zaidi kuugua ambayo ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wanawake wajawazito na wananchi kwa ujumla.

Sera hiyo ililenga kuweka mfumo wa huduma za afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi lengo likiwa kuongeza umri wa kuishi wa Watanzania.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *