Upepo wa mabadiliko unaendelea kuvuma Afrika hasa katika nchi zinazotarajia kufanya uchaguzi siku zijazo. Lakini mabadiliko ya madaraka sio kipimo chautawala bora kwasababu kwa Afrika sura mpya zinazoingia madarakani hazimaanishi mabadiliko ya mfumo wa uongozi.
Changamoto iliyopo ni chaguzi kugubikwa na vitendo vya wizi wa kura, udanganyifu, vurugu za kisiasa na vyama tawala kukataa kuondoka madarakani; zaidi ni kutokuheshimiwa kwa matakwa ya wananchi.
Mwaka huu wa 2018 baadhi ya nchi ikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini, Mali na Libya zinatarajia kufanya uchaguzi wa urais lakini wachambuzi wa siasa za Afrika wanahofia kuzuka kwa mapigano zaidi kwa nchi hizo ikizingatiwa kuwa juhudi za kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani zimekuwa zikitatizwa na baadhi ya viongozi kung’ang’ania madaraka.
Mbio za Urais
Mchambuzi wa siasa za Afrika, Mohamed M Diatta ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sciences Po – USPC cha nchini Ufaransa amesema hali ya kisiasa ya Congo DRC sio ya kuridhisha ikizingatiwa kuwa rais Joseph Kabila ameongeza muda wa kukaa madarakani baada ya kushindwa kuifanyia mabadiliko katiba ambayo ingempa nafasi ya kugombea kipindi cha tatu.
Rais Kabila ameahirisha uchaguzi mara mbili tangu mwaka 2016 alipomaliza muda wake, licha ya kusaini makubaliano na vyama vya upinzani ya kufanya uchaguzi disemba 2017.
Kabila kushindwa kufanya uchaguzi wa urais 2017, kumezua hofu, migomo ya wananchi na shinikizo la ndani na kimataifa wakimtaka aachie ngazi mwaka huu lakini swali linabakiatakuwa tayari kuondoka au atafanya mabadiliko ya katiba ili agombee muhula wa tatu?
Rais Paul Biya (85) wa Cameroon ambaye amekaa madarakani tangu 1982, anatarajia kugombea tena oktaba mwaka huu. Ingawa hakuna dalili za kuachia madaraka, amekuwa akipata upinzani na shinikizo kutoka kwa nchi za Anglophone wakimtaka asigombee tena kwasababu ya kuzoofika kwa afya yake.
Rais wa Congo DRC, Joseph Kabila (kulia) akiteta jambo na rais wa Afrika Kusini aliyeondolewa madarakani, Jacob Zuma hivi karibuni
Madagascar nako, inatarajiwa uchaguzi utafanyika mwishoni mwa mwaka huu huku rais wa sasa Hery Rajaonarimampianina akitarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa watangulizi wake, Marc Ravalomanana na Andry Rajoelina. Kisiwa hicho ambacho kina historia ya kukosa utulivu tangu 2001, inaelezwa kuwa vurugu zinaweza kuzuka tena ikiwa wanasiasa watashindwa kuweka tofauti zao pembeni.
Akihojiwa na gazeti la Conversation, Diatta amesema hali bado tete kwenye nchi tatu za Sudan Kusini, Libya na Mali ambazo zimekosa utulivu wa kisiasa kwa miaka kadhaa iliyopita na huenda hali hiyo ikabadilika na kuwa mbaya zaidi baada ya uchaguzi wa urais utakaofanyika mwaka huu.
Amesema mazungumza ya kurejesha amani katika nchi za Libya na Sudan Kusini hayajatoa matokeo chanya kwa wananchi ambao wanaishi kama wakimbizi. Lakini nchini Mali, serikali imeshindwa kudhibiti mipaka yake kwasababu ya mapigano ya waasi ambao wanashikilia eneo la Kaskazini.
Mchambuzi huyo wa siasa za Afrika amesema haitashangaza kumuona rais wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi kuchaguliwa tena, uchaguzi ukifanyika kwasababu amefanikiwa kudhibiti nguvu za wapinzania wake kwa nguvu za jeshi.
Nchini Chad bado kunafukuta kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambapo uchumi umeharibiwa vibaya. Lakini rais wa nchi hiyo Idris Deby bado ana nguvu ya kuendelea kutawala licha ya waasi kumshambulia mara kwa mara, na anatarajiwa kushinda katika uchaguzi wa bunge utakaofanyika mwaka huu.
Chaguzi hizo zitakazofanyika mwaka huu zitaididimiza zaidi Afrika kwenye mapigano ya kisiasa au itakuwa ni nuru mpya ya kuimarika kwa demokrasia inayozingatia sauti za wananchi na maslahi mapana ya taifa?
Licha ya Afrika kutajwa kwa sifa mbaya ya viongozi wake kutawala kiimla bado ziko nchi chache ikiwemo Kenya na Ghana ambazo zimeonyesha mfano mzuri wa demokrasia ya kupokezana madaraka kwa njia ya amani.
Upepo huu wa demokrasia unaweza kusambaa katika nchi nyingine ikiwa viongozi watasoma alama za nyakati na kuamua kujenga taasisi imara za uongozi na kuruhusu demokrasia kupenya katika nchi zao.