ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameendelea kusakamwa na Jeshi la Polisi.
Katika mazingira yanayoashiria kutokamilika kwa jitihada za kumfungulia mashitaka Askofu Gwajima, Polisi walimkamata jana na kumhoji katika Kituo cha Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na baadaye kwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi.
Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala, ameiambia FikraPevu mapema leo (Jumamosi, Machi 3, 2017) kuwa Gwajima alihojiwa na kufanyiwa upekuzi na baadaye kuachwa njiani.
"Hakuna kitu walichokikamata wala kukiona nyumbani kwa Askofu na hata walipokwenda eneo jingine, hawakukuta kitu," Wakili Kibatala aliieleza FikraPevu.
Anasema baada ya kujiridhisha kuwa hawakupata walichokuwa wakikitafuta, walimuacha njiani bila hata kumrudisha nyumbani kwake, eneo la Salasala, Dar es Salaam.
"Inashangaza hata baada ya kuwa naye na kumpekua nyumbani na maeneo mengine, hawakumrudisha nyumbani kwake, hii ni hatari sana," alilalamika Kibatala katika mahojiano na FikraPevu.
Tangu kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba Askofu Gwajima huenda anahusika katika matumizi au biashara ya dawa za kulevya, Gwajima amekuwa akikemea kuhusishwa kwake na amekuwa akitumia ibada za kanisa lake kulaani wito huo.
Gwajima hata hivyo, baada ya kukamatwa kwa mara ya kwanza, aliachiwa bila masharti yoyote, hali inayoonekana kwamba huenda hana uhusika katika biashara hiyo.
Askofu Gwajima amekuwa akitangaza na kumhimiza Rais Magufuli kumhamisha Makonda kutoka mkoa huo na kumpangia kazi nyingine, kwani "kuongoza Dar es Salaam hawezi."