MITOBOZANO NA UMWAGAJI WA MAJI KATIKA MIGODI MERERANI.

Belinda Habibu

Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwatengea wachimbaji wadogo wa madini maeneo katika migodi mbalimbali ikiwemo ile ya Mererani, ili waweze nao kushiriki katika sekta hii.
Wachimbaji wafanyakazi ,wamiliki wa migodi (wachimbaji wadogo) wa migodi ya Mererani, wanachangamoto nyingi ikiwemo kukosa mitaji ya kuendesha uchimbaji, ongezeko la gharama za vifaa mara kwa mara , na kukosekana kwa mikataba ya kazi kwa wachimbaji wanaoingia migodini.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo pia lipo suala ambalo linawaongezea mzigo wachimbaji wadogo na hata kuhatarisha maisha kwa wachimbaji wafanyakazi ambao huzama chini kuchimba madini husika.
John Eliud ni mchimbaji mfanyakazi wa tanzanite kitalu B, anasema wanapokuwa chini wakichimba, wanaweza wakaona ghafla maji mengi yanayomwagwa na mwekezaji kutoka kampuni ya Tanzanite One, baada ya mitobozano ya ndani kwa ndani.
Ameongeza mchimbaji huyo, unajua tunapokuwa tunachimba tunaweza kukuta maji ,ila huwa sio mengi sana na hayatoki kwa kasi sana, lakini haya yanaonekana kumwagwa na itawalazimu kutoka kwa haraka na ni hatari.
Mchimbaji Mwingine Hashimu Said Nyambi anasema maji huwa yanamwagwa na mwekezaji, yanayotoka chini si ya kasi ile, na kwetu sisi ndio ukata unazidi kwa kuwa itamlazimu mwenye mgodi asimamishe uchimbaji ili atafute mashine za kunyonya maji yote ndio tuendelee.
Hashimu ameongeza kipindi cha kusubiri huwa kinaweza kuwa cha muda mrefu na kutulazimu kwenda mgodi mwingine kufanya ‘bingo’(kibarua cha kutoa mchanga na uchafu wa chini inakochimbwa tanzanite) ili tuweze kuishi tukisubiri mchimbaji mdogo akirekebisha tatizo hilo.
Mwenyekiti wa wanawake wamiliki wa mgodi ya tanzanite Mererani , Stella Shayo alisema walishaenda hadi Dodoma bungeni kuzungumzia suala la maji, lakini bado linaendelea na anayemwaga maji ni huyu mzungu (mwekezaji).
Akizungumzia sababu hasa ya mwekezaji kumwaga maji mwenyekiti huyo anasema,tukiwa tunachimba na tukaingiliana huko chini (mitobozano),na akakuona unapata basi anamwaga maji na itabidi ubaki hapo hapo ulipo ama urudi nyuma.
“Gharama ni kubwa itakulazimu kununua pampu kama za mamlaka ya maji safi na salama, uwe na jenereta kubwa kwa kweli ni gharama”alisema mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa tanzanite Mererani, (MAREMA) Zephania Mungaya alisema kinachotusumbua ni ufinyu wa eneo la vitalu vyetu kuwa mita 50 kwa 50, na tumeambiwa tuchimbe ‘vertical’ kama shimo la choo, lakini miamba ya tanzanite kijiografia unatakiwa uchimbe ‘horizontal’
Mungaya amesema suala la maji, ofisi hii imelishughulikia sana hadi kwa waziri wa madini na akalikabidhi kwa naibu wake ,naye (naibu waziri), akazungumza na mwekezaji (Tanzanite One) kuwa aache kumwaga maji na alifanya hivyo kwa siku mbili lakini mpaka leo anamwaga maji.
Ameongeza alifanya juhudi tena ya kumtafuta waziri na akamjibu akutane na maofisa madini wa kanda kusuluhisha tatizo hilo,na akaenda kwa kamishna msaidizi wa madini kanda ya kaskazini Mhandisi Benjamini mchwampaka na alijibiwa wanamwaga katika maeneo yao ya kimipaka.
“Migodi yote imetobozana hivyo maji yanayomwagwa kwanza yanawasha ukimwagikiwa nayo, pili yanaweza kuozesha miamba mingine na ikioza inaweza ikapasuka na kuwafunika wachimbaji wakiwa chini.”alisema Mungaya.
Kamishna wa madini kanda ya kaskazini mhandisi Benjamini Mchwampaka alisema kitaalamu ukichimba kwa kwenda chini hata shimo la choo utakuta maji, sembuse wao wanachimba umbali mrefu lazima watakuta maji,linalotakiwa hapa ni uwelewa.
Meneja mahusiano msaidizi wa Tanzanite ONE, Halifan Hayeshi alisema si kweli kwamba tunamwaga maji, sisi tuna sehemu tunayomwaga maji na imo ndani ya mipaka yetu, sasa kama wachimbaji wanaingia hadi maeneo hayo basi maji watayakuta.
Ameongeza unajua hakuna kitu kizuri kama kufuata sheria wangechimba katika mipaka ya maeneo yao ili kusiwe na malalamiko.
Sera ya madini ya mwaka 2009, imesema serikali itahakikisha mahusiano mazuri kati ya mwekezaji na jamii inayozunguka mgodi, na taifa kwa ujumla na ushirikishwaji wa jamii ili kufanikisha shughuli nzima ya uchimbaji madini.

Mkukuta wa pili unasema, kutoendelea kwa sekta ya madini hapa nchini kunatokana na sababu mbalimbali ikiwemo uongezewaji mdogo wa thamani kwa madini,mahusiano mabovu ya kimazingira na migogoro,ukosefu wa teknologia na wataalam.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *