Na Juma Ng’oko, FikraPevu – Mwanza
MAMIA ya wakazi wa Jiji la Mwanza pamoja na vitongoji vyake, hasa wanawake wakiwemo askari wa Jeshi la Polisi, jana walifurika kwenye viwanja ya ukumbi wa Gandhi jijini, kwa ajili ya kumpokea mwanamke mwenzao, Maimuna Kanyamala, aliyetuzwa ngao pamoja na cheti cha ujasiri katika kutetea haki za wanawake na wasichana mkoani hapa.
Kanyamala ambaye ndiye Mkurugenzi wa shirika la Kivulini; shirika lisilokuwa la Kiserikali Jijini hapa amepata tuzo ya ujasiri mwaka huu kutoka serikali ya Marekani kutokana na mafaniko katika suala zima la kutetea haki za wanawake na wasichana.
Maandamano hayo yalianzia katika uwanja wa ndege majira ya saa 2 asubuhi hadi Gandhi Hall (majira ya saa 4 asubuhi) kupitia barabara kuu la lami, Airport –Jijini kati na yaliyepokea Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Said Amanzi ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Pamoja na mapokezi hayo , Kanyamala alikabidhiwa mavazi ya kishujaa pamoja na silaha za jadi zinazotumiwa na kabila la Wasukuma, ikiwemo mkuki na ngao ili aweze kukabiliana vyema na wanaume wenye tabia za ukatili dhidi ya wanawake.
“ Wito wangu kwa wanawake ni kwamba ondokaneni na kasumba kwamba mkiwezeshwa mnaweza; kwa hakina ninyi mnaweza hata bila kuwezeshwa na ndiyo maana mwamke mwenzenu Maimuna ameleta heshima ndani na nje ya mkoa wa Mwanza mwaka huu “ alisema Mkuu wa Wilaya wakati akihutubia.
Alifafanua kuwa tuzo hiyo imepatikana kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na mwanamke mwenzao; kazi ambayo ilikubalika ndani na nje ya nchi.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwaasa wanawake wajitume katika kufanya kazi za uzalishaji mali pamoja na mambo mengine, waweze kuheshimika katika jamii.
Amanzi aliwataka wanawake wasifanye mapinduzi ambayo yanaweza kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima baina yao na wanaume kwa kisingizio cha kutetewa kisheria.
“ Ninatoa wito tena kwa wazazi hasa Wasukuma kwamba tafadhali wapeni nafasi za masomo watoto wenu wa kike; na hapo ndipo tutakapopata wajasiri wengi wanawake mkoani mwetu” alisisitiza Mku huyo wa Wilaya.
Alisema baadhi ya wazazi katika kabila la Wasukuma hawathamini elimu kwa watoto wa kike, kitendo ambacho kinawanyima fursa wanawake katika masuala mbalimbali ya maendeleo mkoani hapa.
“ Kwa heshima ya kabila la Wasukuma, ninamkabidhi kwa kumvalisha mkia wa nyumbu ikiwa ni ishara ya mnyama mpole, na pia ninamvalisha ngozi ya ng’ombe ambayo ni ishara ya mnyama ambaye anaishi na binadamu kama rafiki” alisema Mhangwa Mhangwa, wakati akikabidhi zana za kimila na kuongeza kwamba
“ Ninakukabidhi ‘shimbi’ na mkanda wa ngozi kwa ishara kuwa utawaunganisha wanawake na wanaume katika masuala ya kuzuia ukatili; unyoya wa mbuni ni ishara ya ujasiri; ngao kwa ajili ya kujikinga na wenye tabia za upinzani wa harakati hizi pamoja na mkuki kwa ajili ya vita dhidi ya wanaokaidi sheria zinazopingana na ukatili dhidi ya wanwake” alisema Mhangwa huku akishangiliwa na umati wa wanawake.
Kwa upande wake, Kanyamala aliishukuru serikali ya Tanzania ambayo ilishirikiana bega kwa began a serikali ya Marekani kwa ajili ya maandalizi ya tuzo hiyo.
Alisema tuzo hiyo imetolewa na ubalozi wa nchi ya Marekani, Balozi Altonso Lenhardt.
Kanyamala alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake wenzake washirikiane na shirika la Kivulini pamoja na serikali kwa ajili ya kuwaelimisha wanaume ili wabadilike na kuchukia vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.