WATU saba wanaosadikiwa kuwa ni majambazi yaliyokuwa na silaha za moto, yamevamia na kuuteka kwa saa kadhaa mji wa Itabagumba, Wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Inadaiwa kwamba, tukio hilo lilitokea majira ya saa 8 usiku wa kuamkia leo, baada ya majambazi yanayotajwa kufikia saba kuvamia nyumba moja ya wakala wa huduma ya M-PESA, katika mji mdogo wa Mbugani Senta Itabagumba, ambapo yalijibizana kwa risasi za moto na walinzi wa kampuni binafsi.
Mashuhuda wa tukio hilo kutoka Itabagumba, walimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba, siku hiyo majambazi hayo yakiwa yametanda eneo la mji huo, yalivamia kwenye nyumba hiyo ya wakala wa M-PESA, kisha kupora fedha na kumbaka mwanamke mmoja katika nyumba hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, wakati majambazi hayo saba yakijibizana kwa risasi na askari wa kampuni binafsi, jambazi moja aliyetajwa kwa jina moja la Juma, alipigwa risasi za miguuni na askari wa kampuni binafsi ya Mass Security Guard Ltd, kisha kufariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi.
“Tukio lilikuwa hivi, majambazi yalivamia na kupovunja mlango kwa kutumia fatuma. Na yalipoingia ndani ya nyumba ya wakala wa M-PESA, yalimbaka mfanyakazi wa huduma hiyo, na kupora fedha!.
“Wakati yakivamia, walinzi wa kampuni binafsi waliopo hapa Mbugani Senta, walifyatua risasi hewani na majambazi nayo yakajibu mapigo. Askari kwa ujasiri wao mkubwa wakanyemelea yaliko na kumimina risasi na jambazi moja likafa”, alisema shuhuda mmoja wa tukio hilo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbugani A lilipotokea tukio hilo, Amani Musa alitthibitisha jana kwa njia ya simu yake ya kiganjani, ambapo alimtaja wakala huyo wa huduma ya M-PESA kuwa ni Kiliza Simon, ambaye amepanga kwenye nyumba inayomilikiwa na Abdul Yusuf Njunwa.
“Ni kweli majambazi saba yalivamia usiku leo, hapo kwa Kiliza Simon…lengo yalitaka kupora fedha. Yalimbaka mwanamke na kumuumiza vibaya sana.
“Tunashukuru askari wetu wa kampuni binafsi ya Mass Security walipambana na majambazi haya na kufanikiwa kulipiga risasi jambazi moja, lakini baadaye limekufa”, alisema mwenyekiti huyo wa Kitongoji cha Mbugani A, Musa.
Hata hivyo, alisema kabla ya kufariki jambazi hilo liliwaambia kwamba, huwa limekuwa likifanya matukio hayo ya ujambazi kwa maeneo tofauti, na kwamba lilifika Itabagumba juzi jioni likitokea kijiji cha Kanyara, na kwamba majambazi wengine walikimbia na bunduki walizokuwa nazo.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema: “Nipo safarini, sina taarifa kama hizo. Lakini nashukuru kwa taarifa, ngoja nifuatilie nitakujulisha”.
Mwishoni mwa Novemba mwaka huu, watu 12 wanaosadikiwa kuwa majambazi yakiwa na silaha za kivita, yalivamia na kuteka Kisiwa cha Kome Wilayani Sengerema mkoni Mwanza, kisha kupora fedha zinazodaiwa kufikia mamilioni 20.
Mbali na tukio hilo, hivi karibuni majambazi matano yalivamia katikati ya jiji la Mwanza majira ya saa 2 asubuhi, ambapo yalijibizana kwa risasi za moto na askari polisi kabla ya kuuawa.
Tukio jingine la jaribio la kutaka kupora lilifanyika maeneo ya Liberty katikati ya jiji majira ya jioni, ambapo polisi walisema majambazi hayo yalikuwa yakijiandaa kwenda kufanya uhalifu maeneo ya Nyegezi.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza