MWANZA IJUMAA APRILI 6, 2012: HATAMAYE Jeshi la Polisi mkoani hapa limeanza kuwakamata na kuwahoji watumishi wa idara ya ardhi katika halmashauri ya jiji la Mwanza; ili siku yoyote wapandishwe kizimbani kujibu tuhuma za kukaidi amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba.
Watumishi hao ni sehemu ya watuhumiwa wengine zaidi ya kumi ambao
inadaiwa kwamba Novemba 23 mwaka jana katika mtaa wa Pasiansi Mashariki jijini hapa wakiwa na nyundo pamoja na mapanga walivamia na kuvunja nyumba ya mjane mmoja, Moshi Mzungu(67) ambayo ipo katika kiwanja ambacho mgogoro wake ulikuwa haujafikiwa maamuzi mahakamani.
Hata hivyo, watumishi hao wamehojiwa huku mtumishi mwenzao ( katika idara hiyo), Asubuhi Otieno, akiwa nje kwa dhamana baada ya kutiwa hatiani mwezi uliopita kwa kosa la kuwasilisha ushahidi wa uongo mahakamani.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la Polisi jijini hapa kimeliambia FikraPevu kwamba tayari polisi limeshawahoji watumishi 5 kati ya 7 ambao Februari mwaka huu walipatikana na kosa la kupuuza amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba.
Waliohojiwa wametajwa kwamba ni Victor Mashamba, Kitia Kagoroba, Abdon Baraka pamoja na Lazaro Matulanya ambaye alikuwa dereva wa gari pamoja na mfanyakazi mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Kassim.
Habari zinadai watuhumiwa wengine wawili (Mwita Wambura pamoja na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mwita) wanatarajiwa kukamatwa na kuhojiwa wakati wowote.
Watuhumiwa hao wamekamatwa ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa barua
yenye kumbukumbu namba DLHT/NZ/APP namba 244/2010; barua ya Februali 17 mwaka huu ambayo iliandikwa na kusainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba mkoa wa Mwanza, Christian Mwashambwa.
Inadaiwa kwamba barua hiyo iliyotumwa kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai wa Mkoa(RCO) wa Mwanza (Fikra Pevu limepata nakala yake) inasema kwamba kwa makusudi watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma pamoja na mali za umma katika kutekeleza azima zao ovu.
Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Barlow, zinasema kwamba watu hao walihojiwa kwa nyakati na siku tofauti mwezi uliopita.
“ Siyo kwamba polisi tumekaa kimya ama tunawaogopa watumishi wenzetu wa serikali walioamriwa kukamatwa kutoka ofisi za halmashauri ya Jiji la Mwanza; hapana, kazi imeanza na tayari watano wao wameshahojiwa,” kilidai chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa zoezi la kuwakamata watuhumiwa hao limechelewa kutokana na kughubikwa na mizengwe kutoka kwa baadhi ya wanasiasa pamoja na maafisa kadhaa wa polisi mkoani hapa ambao wamekuwa wakiwakingia kifua watuhumiwa hao.
Kwa mujibu wa habari, askari hao wanaodaiwa kutokuwa waaminifu waliwasilisha taarifa zilizokuwa zikipingana na amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba mkoani hapa.
“Mimi nilishatoa maelekezo kwa RCO ( Mkuu wa Upelelezi wa Jinai wa Mkoa) ili watuhumiwa hao wakamatwe na kuhojiwa na kisha wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi,” alithibitisha Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Liberatus Barlow.
Kamanda huyo alisema ofisi yake inaheshimu sheria za nchi na kwamba haifanyi kazi kwa kushinikizwa na wanasiasa wala watendaji wengine serikalini.
Amri ya kuwakamata watumishi hao pamoja na watu wengine waliohusika katika kubomoa nyumba namba 410 iliyoko Kitalu L Pasiansi Mashariki B ilitolewa Februali mwaka huu.
Imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza
wakitoka huko waje dsm, waone ardhi palivyojaa madudu