Serikali kutatua Tatizo la Wachimbaji wadogo?

David Azaria

WIZARA ya Nishati na Madini imetangaza kutatua tatizo la wachimbaji wadogo kukosa maeneo maalum ya uchimbaji na kwamba tatizo hilo linatarajiwa kupungua kama sio kumalizika mwaka 2015.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini Steven Masele amelithibitishia wa Habari hii kwamba kwa sasa Wizara hiyo imejielekeza katika kutatua migogoro ya wachimbaji wadogo kwa kuhakikisha kwamba wanakuwa na maeneo maalum ya uchimbaji kama ambavyo serikali inafanya kwa wawekezaji wakubwa.

Anasema Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 1.5 ambao wanategemea uchimbaji mdogo,wakati ambapo makampuni makubwa ya uwekezaji kwenye sekta hiyo yamefanikiwa kuajiri watu 15,000 pekee jambo ambalo linathibitisha kwamba yanahitajika maeneo mengi maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

“Suala la kutenga na kugawa maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji  wadogo ni mwendelezo hauna kikomo kwa sababu tunaamini kwamba  kila wakati watakuwa wakijitokeza wachimbaji wakiwa na mahitaji  ya maeneo ya kuchimba,Lakini kwa hawa ambao tumeanza nao tangu mwaka mwa 2007 tunatarajia kukamilisha zoezi la kuwapatia maeneo ya kuchimba kabla ya mwaka 2015’’.anasema Waziri Masele.

Hata hivyo huenda ahadi hiyo ya serikali isifanikiwe kutokana na kasi ya utengaji wa maeneo hayo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo kuwa ndogo,ikilinganishwa na idadi ya wachimbaji wanaohitaji maeneo hayo,huku serikali ikionekana kuwajali zaidi wawekezaji wakubwa kwa kuwapatia maeneo makubwa.

Kwa mfano katika Mkoa wa Geita ambapo inaelezwa na Ofisa Madini Mkazi Juma Sementa kwamba kuna wachimbaji wadogo wapatao 300,000 hadi kufikia mwezi wa 10 mwaka jana (2012) ni wachimbaji wadogo 100,000 tu ndio walikuwa wametengewa maeneo maalum ya uchimbaji.

Hata hivyo baadhi ya wananchi hususani wachimbaji wadogo wamepata hofu kwamba huenda Serikali kupitia Wizara hiyo imeonesha nia ya kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo kwa sababu imeona uchaguzi mkuu umekaribia,na kwamba huenda baada ya uchaguzi huo kukamilika mwaka 2015 kabla ya zoezi hilo kukamilika halitakamilishwa.

Akizungumzia madai kwamba serikali imeamua kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo yenye migodi kama vile Geita kwa sababu imekuwa ikikabiliwa na upinzani kwenye chagauzi mbalimbali ukiwemo uchaguzi mkuu,Masele anasema hayo ni maoni ya watu na serikali haiwezi kulijadili hilo.

“Hayo ni maoni yao ambayo yanaweza kuwa kweli ama uongo,lakini moja ya kazi ya serikali ni kuhakikisha kwamb inatatua matatizo yanayowakabili wananchi wake kadri ionavyo,kwa hiyo sisi tunachofanya hapa ni kutekeleza wajibu wetu kwa wananchi sasa kam kuna mtu anona kwamba tunafanya hivyo ili kujiandaa na uchaguzi mkuu sawa kwa sababu pia tunaamini tusipotekeleza matakwa ya wananchi hawatatupa nafasi ya kuendelea kuwa madarakani….’’anasema Waziri Masele.

Katika Mkoa wa Geita ambapo zoezi hilo la utengaji wa maeneo ulianza tangu mwa 2007 hadi kufikia mwezi wa 11 mwaka jana ulikuwa umefanikiwa kutenga eneo la Mgusu katika kata ya Mtakuja lenye ukubwa wa Hekta za mraba 75 ambapo zaidi ya wachimbaji wadogo 9000 wamejiunga kwenye kikundi na kuanza uchimbaji.

Eneo lingine ambalo pia serikali imefanikiwa kutenga  na kutoa viwanja  53 ni katika maeneo ya Lwamgasa na Nyarugusu ambapo zaidi ya wachimbaji wadogo 90,000 wamepata maeneo ya uchimbaji,awali maeneo hayo yalikuwa yakimilikiwa na wawekezaji wakubwa hali ambayo ilikuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara baina ya wachimbaji hao na wawekezaji wakubwa.

Katika eneo la Mgusu mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Nestory Joseph anasema kwa muda wa miaka minane wamekuwa na mgogoro mkubwa kati yao na mwekezaji mkubwa ambaye ni Kampuni ya Shanta Mine Ltd ambaye alichukua eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji na kuwafanya wao kukosa eneo la uchimabji..

Anasema walianza shughuli za uchimbaji mdogo katika eneo hilo mwaka 1987 kwa kumiliki eneo hilo kama eneo la wachimbaji wadogo ambapo mwaka 1990 eneo hilo lilichukuliwa na likawa linamilikiwa na mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Chipaka.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo Amri ya kurejeshewa eneo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda Septemba 10 mwaka jana aliyefanya ziara ya kuwatembelea wachimbaji hao.

Wachimbaji wadogo wa eneo la Mgusu wanasema kutolewa kwa eneo hilo kwa kwa ajili ya shughuli zao za uchimbaji mdogo kumeleta faraja kwao kutokana na kukosa eneo maalum kwa ajili ya shughuli zao za uchimabaji.kwani kutokana na kukosa eneo la uchimbaji kuliathiri uchumi wao kwa kwa kiwango kikubwa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo yao.

Mmoja wa wachimbaji hao Michael Malebo anasema eneo la Mgusu lilikuwa ni eneo lao kama wachimbaji wadogo kwa vile wao ndio waliobani uwepo wa dhahabu na kisha baadaye kuamua kuanzisha kijiji kwa mujibu wa sheria ili kulifanya eneo hilo kutambulika kama eneo la wachimbaji wadogo.

Kauli ya Malebo inaungwa Mkono na wenzake Jacob Madirisha na Matutu Henry ambao wanaongeza kwamba kabla ya Kunyang’anywa eneo hilo na kupewa mwekezaji huyo walikuwa wakifanya shughuli zao kwa amani na utulivu na kufaidika uchimbaji mdogo uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo.

Wanasema baada ya kukabidhiwa eneo hilo wameamua kuanzisha chama cha ushirika kama ambavyo wameshauriwa na serikali,ili kuhakikisha kwamba wanaendesha uchimbaji wenye tija,lakini pia ikiwa ni njia mojawapo itakayowafanya kunufaika na mikopo ya fedha ama vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi kutoka kwenye mabenki pmoja na taasisi mbalimbali.

Wanabainisha kwamba hadi kufikia katikati ya mwezi wa kumi mwaka huu tayari chama hicho chenye usajili MZR 1609 kilikuwa na wachama 115 ambao ni wakai wa kijiji hicho huku katibu Mkuu wa chama hicho Mohamed ibrahimu akisema kwamba hakuna mtu yeyote kutoka nje ya wakzi wa kijiji hicho ambaye ataruhusiwa kujiunga na cham hicho.

Ofisa Madini Mkazi Mhandisi Sementa anasema serikali ilianza kutenga maeneo malum kwa ajili ya wachimbaji wadogo Mkoani Geita mwaka 2011 ambapo ilitenga maeneo ya Lwamgasa na Nyarugusu na kupatikana jumla ya viwanja 53.

Kuhusu eneo la Mgusu ambalo limekabibidhiwa rasmi hivi sasa kwa wachimbaji wadogo na serikali,idara ya madini tayari imeuagiza uongozi wa ushirika ulioundwa kuhakikisha kwamba wataalamu wanaajiriwa kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.

"Hawa watu wa Mgusu tayari serikali imewakabidhi eneo hili kwa ajili ya shughuli za uchimbaji kama ambavyo wameomba kwa muda mrefu,kwa sababu tayari wameunda ushirika wao na kupata usajili hatutarajii tena kwamba watakuwa na shughuli za uchimbaji mdogo,tunatarajia uchimbaji wao utakuwa ni wa kati ambao utawawezesha kupata uzalishji mkubwa……'' anasema Mhandisi huyo na kuongeza.

Kwa mujibu wa mhandisi huyo pamoja na maeneo hayo kutengwa lakini bado kuna idadi kubwa ya wachimbaji ambao bado hawajapata maeneo maalum kwa ajili ya uchimbaji,na kwamba kutokana na hali hiyo tayari idara hiyo imetuma maombi kwa Kamishna wa madini nchini ili kutenga jumla ya Hekta 3,782.6 kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Anasema Mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na wachimbaji wadogo wasiopungua 300,000 ambapo ambao wamepata maeneo maalum kwa ajili ya uchimbaji hawafiki 100,000 hivyo upatikanaji wa Hekta hizo kutatua tatizo la upungufu wa maeneo ya wachimbaji wadogo.

Maeneo ambayo tayari idara hiyo imeomba kibali kutoka kwa Kamishna wa madini nchini ili kutenga kuwa maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni Lwenge,Kanza,Bukolwa,Nyarugusu,na Busolwa wilayani Geita,Kasubuya Wilayani Nyangh'wale,na Ng'anzo na Shenda wilayani Bukombe,na kamba kutengwa kwa ameneo ya Nyantimba wilayani chato na Matabe wilayani Biharamulo kutafanyika baada ya kupatikana kwa vibali vya idara ya misitu kwa kuwa maeneo hayo yamo ndani ya misitu ya hifadhi.

Baadhi ya wachimbaji wameonesha wasiwasi wa zoezi la utengaji wa maeneo malum kwa ajili yao kwamba huenda limeshika kasi hivi sasa kutokana na serikali kupata wasiwasi wa kupata kura kwenye maeneo ya madini kama eneo la Geita ambapo kumekuwepo na upinzani mkubwa kwa serikali ya CCM na hasa wakati wa uchaguzi.

“Serikali ya CCM imekuwa ikipata msukosuko mkubwa wa kunyimwa kura wakati wa chaguzi mbalimbali,sasa yawezekana wameamua kuwa na kasi kubwa ya upatikanaji wa maeneo kwa ajili yetu ili tuje tuwapatie kura kwenye chaguzi zinazokuja,jambo ambalo linatupa mashaka kwamba kama zoezi halitakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 baada ya hapo tunaweza tusipate maeneo hayo….’’ anasema Enock Malima mchimbaji katika eneo la Lwamgasa.

Deo Joseph, Mabula Kidilya, na Joseph Kadiso wanasema serikali ilitangaza kuwatengea maeneo tangu mwaka 2008 lakini imeichukua miaka mitatu kuanza kutekeleza zoezi hilo,ambapo hadi sasa ni wachimbaji wapatao 100,000 waliopatiwa maeneo huku zaidi ya 300,000 wakiwa bado.

“Labda kwa sababu uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu umekaribia ndio maana wamekuwa na kasi ya kututengea maeneo,wasiwasi wetu ni kwamba kama chaguzi hizi zitapita bila zoezi kukamilika maana yake ni kwamba hatutayapata hayo maeneo….anasema mmoja wa wachimbaji hao Mabula.

Uchunguzi wa Mwandishi wa makala haya umebaini kuwa maeneo ya uchimbaji wa madini kwa mfano katika Mkoa wa Geita yamekuwa yakikabiliwa na upinzani mkubwa katika chaguzi mbalimbali ukiwemo uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2010,ambapo jimbo la Bukombe lilichukuliwa na CHADEMA huku lile la Geita likiponea Chupuchupu.

Hata hivyo Madai hayo yanapingwa vikali na Naibu Waziri wa Nishati Masele akisema kwamba kazi ya serikali ni kuhakikisha kwamba inatatua kero zinazowakabili wananchi wake,hivyo utengaji wa maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni mpango wa muda mrefu wa serikali ambao umeanza kutekelezwa.

“Wanachokifanya wapinzani ni kuangalia wapi ambapo serikali haijatekeleza ndio inachukuwa na kwenda kuwaeleza wananchi,na sisi kama serikali tunachofanya ni kuhakikisha kwamba tunatatua kero za wananchi kadri tuwezavyo…’’ anasema.

Anaongeza“na hili sisi kama Wizara ya Nishati na madini tumebaini kwamba ni moja ya kero kubwa kwa wachimbaji wadogo na hasa katika mkoa wa geita ndio mana tumeliwekea mkazo kuhakikisha tunalitatua kabla ya mwaka 2015,pamoja na kwamba litakuwa mwendelezo”.

Mbali na mafanikio yaliyokwishapatikana katika suala la kutatua kero za wachimbaji wadogo bado kuna changamoto nyingi katika sekata hiyo,ikiwa ni pamoja na wananchi kutozongatia sheria na kanuni za madini kama vile kutoona umuhimu wa kulipia leseni katika maeneo yao ya uchimbaji hali ambayo imekuwa ikiwasababisha kupoteza maeneo yao pindi wanapojitokeza wawekezaji wakubwa.

Bado serikali kupitia Wizara hiyo haijatoa mafunzo mahususi kwa wachimbaji wadogo ili kufahamu umuhimu wa kuchukua leseni za kumiliki maeneo ya uchimbaji,jambo ambalo linawanyima haki wachimbaji hao.

Suala la ukosefu wa mitaji kwa wachimbaji wadogo nalo linaonekana kuwa ni tatizo kubwa ambalo serikali haijalipatia ufumbuzi wa uhakika,ambapo pamoja na kuwepo kwa mfuko wa kuwawezesha wachimbaji wadogo chini ya serikali lakini mfuko huo bado haujafanya kazi yake sawasawa kwa mujibu wa malengo ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo ya vifaa vya uchimbaji kwa wachimbaji.

Ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanaondokana na changamoto hizo ni vyema serikali ikaendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na wachimbaji wadogo,ili kuwaelewesha jamii taratibu za kuomba maeneo kwa ajili ya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini,sanjari na kuboresha mfuko wa wachimbaji ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata mitaji kwa ajili ya shughuli zao.

1 Comment
  • ni vema wana siasa waache upinzani na washirkiane ili kuleta maendeleo ya kiuchumi huko mkoani geita

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *