Sumaye, Lowassa, Ridhiwani na Warioba uso kwa uso Bunda

Jamii Africa

WAZIRI  wa Uhusiano na Uratibu  katika  ofisi ya Rais, na Mbunge wa Bunda Stephen  Wassira atakua mgeni rasmi  katika harambee  itakayohudhuriwa pia na wanasiasa kadhaa nchini.

Baadhi ya wanasiasa walioalikwa wanatajwa kuwa ni mawaziri wakuu wastaafu Fredrick Sumaye na Jaji  Joseph Warioba na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowasa pamoja na  mtoto wa Rais Ridhiwani  Kikwete.

Harambee hiyo imeelezwa ni ya kuchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati, ujenzi  wa nyumba  za walimu pamoja na vyumba  vya madarasa  shule za serikali katika  kata ya Nyamuswa, Bunda  mkoani Mara, ambako Wassira ni Mbunge wake.

Taarifa hiyo  imetolewa  na  Mwenyekiti wa Wazee wa Kamati ya Maendeleo ya Elimu  katika Kata ya Nyamuswa, Wilfred  Sinduka, ambaye anasema harambee  hiyo  itafanyika Januari  8 mwaka huu  katika  shule ya msingi  Nyamuswa;  shule  ya msingi  alikosoma Jaji Warioba.

“Harambee  hiyo  itaanza saa 4  asubuhi  ambapo Ridhiwani  Kikwete  pamoja na Waziri  wa Uhusiano na Uratibu  katika ofisi ya Rais, Stephen  Wassira  wamealikwa “  alisema  mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo  alisema  lengo  la harambee hiyo ni kupatikana kiasi cha zaidi ya  shilingi  milioni 150  .

Alifafanua kuwa  fedha  hizo zitatumika  katika ununuzi wa madawati 816  yanayohitajika katika  shule zote za msingi(za serikali) pamoja na ujenzi wa nyumba pamoja na vyumba vya madarasa katika sekondari  zilizomo  katika kata ya  Nyamuswa.

Alisema  wazo  la harambee hilo  lilitokana na msaada wa madawati  30  yaliyotolewa  na  mmoja  wa wanafunzi waliowahi  kuhitimu elimu ya msingi katika  shule ya msingi Ikizu  iliyomo ndani ya kata ya Nyamuswa, Juma Makongoro.

Alisema  mbali  na msaada  huo wa Makongoro   ambaye  sasa hivi ni  Afisa  Uvuvi Mwandamizi  mkoani  Mwanza, bado kuna upungufu  wa madawati katika shule mbalimbali za  msingi  katika kata hiyo.

“Hata  hivyo, tumewaalika  wabunge  wote  wa majimbo  ya mkoa  wa Mara, Viongozi wa serikali, wafanyabiashara  pamoja na  wananchi  mbalimbali  kutoka  ndani na nje ya mkoa  wa Mara”   alisema.

Habari hii imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza

6 Comments
  • Sasa hapo Ridhiwani anakwenda kwenye harambee kama nani kiongozi wa chama ama serikali ?

  • Toka enzi za Nyerere, Mwinyi, Mkapa hatujawahi kusikia watoto wao kuhusishwa na mambo kama haya. Sasa huyu bwana mdogo Rizwani ni kiongozi wa chama, serikali ama kikundi gani hapa Tanzania?.

  • LOWASSA ndiye anayefaa kugombea uraisi ndani ya CCM kwani ni mtendaji aliye makini na anajua nini anafanya,

  • pamoja na kashfa zote anazotajiwa huyu bwana edo lakini bado ndio kichwa tunachokiona ila tunamuomba ajirekebishe kama ni kweli yanayosemwa kwani kwenye siasa kusemwa kupo sana

  • Hivi ninyi mliomwalika Ridhiwan mna maana gani ? kwa sababu mmewaita walio kuwa viongozi na huyo bwana mdogo ili iweje?hata kama nia yenu ni pesa lakini kwa hapo……….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *