Tafiti, teknolojia kukuza biashara Afrika Mashariki

Jamii Africa

Nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa nchi zenye gharama kubwa za uchukuzi na usafirishaji wa mizigo duniani. Gharama hizo kwa kiasi kikubwa zimepunguza ushindani wa bidhaa zinazosafirishwa kutoka maeneo ya pembezoni kwenda katika mataifa ya nje. Pia zimepunguza ukuaji wa biashara na uchumi, utengeneza wa ajira, lakini kiwango cha umaskini kinazidi kuongezeka.

Benki ya Dunia (WB) imekadilia kuwa gharama kubwa za usafirishaji wa mizigo zinapunguza kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa asilimia 1 kila mwaka na inagharimu asilimia 40 ya manunuzi ya walaji ndani ya jumuiya na nchi majirani. Kutokana gharama kubwa za usafirishaji zaidi ya watu milioni 250 wanaathirika kwa namna moja ama nyingine katika maendeleo.

Afrika Mashariki ina njia kuu mbili za biashara ambazo ni sawasawa na asilimia 98 ya biashara zote zinofanywa katika ukanda huu. Mlango wa kaskazini unabeba asilimia 73 ya biashara zote za ukanda huu kuanzia Bandari ya Mombasa ikipitia Uganda mpaka Rwanda, Burundi na Congo (DRC), na kuunganisha nchi za Sudan ya Kusini na Ethiopia.

Pia mlango wa mkuu ambao ni asilimia 25 ya biashara yote ya kanda, ambapo huanzia katika bandari ya Dar es salaam kwenda Rwanda, Burundi and eneo lote la Maziwa makuu.

Bandari ya Dar es salaam

Utafiti wa hivi karibu katika mlango mkuu wa Kaskazini unaonyesha kuwa gharama za uchukuzi wa mizigo katika Afrika Mashariki hugharimu asilimia 42 ya thamani yote mizigo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kuufanya ukanda huu kuwa pili duniani kuwa na gharama kubwa za usafiri na uchukuzi.

Gharama hizo kubwa za uchukuzi ni matokeo ya utendaji duni wa sekta ya usafiri na uchukuzi miongoni mwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki. Nchi hizi bado zinakabiliwa na miundombinu mibovu ya barabara na reli, urasimu wa sera na sheria, teknolojia ndogo ya usafiri, viwango tofauti vya ushuru na forodha ni miongoni mwa sababu chache zinazodhohofisha ukuaji wa biashara.

Kwa msingi huo kati ya nchi 155 zilizofanyiwa utafiti; Afrika Kusini, Tunisia na Misri ndizo zinawekwa katika nchi zenye viwango vya juu katika sekta ya uchukuzi barani Afrika.

Lakini nchi za Afrika Mashariki zina madaraja mchanganyiko ambapo Tanzania inashika nafasi 88, Kenya ya 122 zikifuatiwa na Rwanda na Burundi katika nafasi ya 139 na 155.

Wadau wa masuala ya uchumi wanaonya kuwa kama vikwazo vya ukuaji wa sekta ya uchukuzi havitaondolewa basi rasilimali za Afrika Mashariki zitaendelea kupotea na kuharibika kwasababu hazitumiki ipasavyo. Biashara za nchi nyingine za ngambo zitapungua kwasababu ya gharama kubwa za uchukuzi wa mizigo katika bandari na stesheni za reli.

Pamoja na kuwa changamoto hizi za uchukuzi, wadau mbalimbali wamendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kukuza biashara katika ukanda wa Afrika Mashaki na nchi nyingine ili kukuza kiwango cha uchumi na maendeleo kwa wananchi wa kawaida.

Kwa kutambua hilo, taasisi ya Alama ya Biashara Afrika Mashariki (TMEA) kwa kushirikiana na nchi za ulaya wameanzisha mfuko maalumu utakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali za uchukuzi kwa kutumia utafiti na ugunduzi wa njia bora za kuimarisha sekta ya uchukuzi ili kukuza biashara barani Afrika.

Mfuko huo unajulikana kama Ufumbuzi katika Sekta ya uchukuzi na Usafirishaji (Logistic Innovation for Trade (LIFT) Fund) unalenga kuibua mbinu mbadala za kisayansi zitakazosaidia kutatua tatizo la usafiri wa mizigo ambalo limekuwa kikwazo cha kukua kwa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tumepiga hatua kubwa katika kupunguza gharama za uchukuzi na usafiri katika ukanda huu kwa njia za ufumbuzi. Mfuko unatarajia kutafuta njia mbadala zitakazoinua ushindani wa biashara ambao utachangia mafanikio ya jumuiya ya Afrika Mashariki”. inaeleza ripoti ya mfuko huo.

Malengo ya mfuko ni kupunguza mda mwingi unaotumika kusafirisha bidhaa katika milango mikuu ya Afrika Mashariki na kuchangia katika malengo ya TMEA ambayo yanakusudia kupunguza mda wa usafiri katika milango mikuu ya usafirishaji kwa asilimia 15 ifikapo mwaka 2016.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ikiwa sekta ya uchukuzi na usafiri ya Afrika Mashariki haitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mafanikio ya biashara katika nchi hizo hayatafanikiwa na kukua katika viwango vya kimataifa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi mojamoja za ukanda huu ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi za umaskini.

Magari ya mizigo katika nchi za  Afrika Mashariki

Afrika ya Mashariki hasa Tanzania inatajwa kuwa nchi ya kwanza kati ya nchi 10 Afrika zenye mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli ni ya muhimu sana kuimarisha mshikamano na umoja uliopo katika nchi tano za jumuiya hiyo ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Sudan ya Kusini na Burundi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sekta Binafsi Afrika Mashariki, Lisa Karanja akihojiwa na vyombo vya habari hivi karibuni alisema mfuko huo mpya unalenga kuinua sekta binafsi katika uwekezaji kwa kuondoa changamoto za teknolojia ambazo zitaleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi na kukuza ushindani wa biashara katika jumuiya. 

Anaongeza kuwa mfuko huo utachochea na kuendeleza ufumbuzi na tafiti mbalimbali ambazo zitatengeneza mfumo wa kompyuta utakaotumika katika malori ya mizigo, zaidi mfuko huu umedhamiria kuibadilisha jumuiya hii kuwa kituo kikuu cha uzalishaji wa uchumi katika bara la Afrika.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inatakiwa kutafuta njia mbadala za kutatua changamoto za kibiashara na kuufanya ukanda huu kuwa na ushindani wa kweli.

Kupitia mpango huu ambao unalenga kutatua changamoto za usafiri inakisiwa ifikapo 2015 matatizo ya uchukuzi yatakuwa yamepungua kwa asilimia 15 na upande wa pili biashara ya bidhaa mbalimbali na matafa ya kigeni itakuwa na kuleta tija kwa wananchi.

Ili mipango yote itimie inahitajika nguvu ya pamoja itakayowakutanisha wadau wote wa uchumi na siasa ili kuweka mikakati endelevu itakayounda chombo maalumu cha kusimamia utekelezaji wa malengo ya jumuiya ya Afrika Mashariki katika sekta ya usafiri na uchukuzi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *