Serikali ya Kenya imesema itazuia bidhaa za Tanzania kuingia nchini mwake baada ya Mamlaka ya forodha kuendelea kutoza ushuru kwa bidhaa zinazotengenezwa kwa sukari kutoka nchini humo.
Bidhaa hizo za sukari ni pamoja na keki, juisi, pipi, chokoleti na pipi za kutafuna ambazo huingia nchini na kutozwa ushuru wa forodha. Inaelezwa kuwa Tanzania imekuwa ikiilalamikia Kenya kwamba haitumii sukari inayozalishwa ndani ya badala yake inaagiza kutoka nje ili kutengeneza bidhaa hizo.
Mamlaka za Tanzania zimepewa hadi mwisho wa mwezi huu Mei kutembelea kampuni za Kenya ili kubaini kama zinaagiza nje sukari ya viwandani. Hayo yanatokea wakati nchi hizo mbili zikiwa hazijatatua migogoro mingine ya kibiashara.
Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa Tanzania inatoza asilimia 25 ya bidhaa zinazotoka Kenya hasa zinazotengenezwa kwa sukari, ikiwa zitatumia sukari kutoka nje ya nchi.
Ripoti ya kikao cha Marais John Magufuli na Uhuru Kenyatta kilichofanyika April, 2018 kiliitaka Tume ya Uhakiki ya Tanzania kufika Kenya ili kujiridhisha juu ya matumizi ya sukari ya viwandani inayosemekana inaagizwa nje.
“Tume ya Uhakiki ya Tanzania itafika Kenya kuhakiki matumizi ya sukari ambayo haitozwi ushuru kwenye bidhaa zake na itakamilisha kazi hiyo ndani ya wiki mbili (May 31,2018). Kushindwa kufanya hivyo itasababisha kuchukuliwa kwa hatua za malipizo,” alieleza ripoti ya kikao cha marais.
Pia wazalishaji wote wa bidhaa za sukari nchini Kenya wametakiwa kuipa ushirikiano Tume hiyo ili kukamilisha kazi yake kwa wakati na kutoa mrejesho kwa viongozi wakuu.
Kukataliwa kwa vyeti vya uhakiki
Kwa mujibu wa Jalida la The East African, Tanzania imekataa kupokea vyeti vya uhakiki wa bidhaa vinavyotolewa na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) na kuamua kutoza asilimia 25 bidhaa za sukari za Kenya.
Kimsingi, Vyeti hivyo vinaambatana na nyaraka muhimu zinazoonyesha bidhaa ilikotoka na kiasi cha ushuru kinachopaswa kutozwa ili kuendana na makubaliano ya ya kibiashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Soko la pamoja la Afrika Mashariki linaundwa na nchi tano za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda ambapo zinaruhusu bidhaa zilizotengenezwa ndani ya nchi zao kuuzwa katika nchi yoyote ya jumuiya hiyo bila kutozwa ushuru.
Mamlaka za mapato za Uganda na Tanzania zinawalalamikia wazalishaji wa Kenya kuvuruga ushindani wa kibiashara kwa kutumia sukari ya viwandani inayoagizwa nje ya nchi.
Nchi za Afrika Mashariki hazizalishi sukari ya viwandani zinategemea kuagiza kutoka nje ya jumuisha hiyo. Kenya nayo imezishutumu nchi hizo mbili kwamba zinatumia ushuru wa forodha kuzuia ukuaji wa biashara ndani ya Afrika Mashariki.
Chama cha Wazalishaji cha Kenya (KAM) kilieleza mwezi April kuwa wakati Uganda umelegeza msimamo wake, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) imekataa kukubali kuwa kampuni 14 zinazotengeneza bidhaa za sukari hazifaidiki na biashara hiyo.
“Kuzuiwa kwa bidhaa za Kenya kuingia Tanzania kumeendelea licha ya KRA kuingilia kati na kufafanua jambo hilo kwa majirani zetu Tanzania,” alinukuliwa mmoja wa wazalishaji nchini Kenya, April 26.
Hata hivyo, Tanzania inasubiri majibu ya Tume ya Uhakiki ili iweze kujiridhisha na kuendelea kufanya biashara katika ushindani ulio sawa.
Wachambuzi wa masuala ya kibiashara wametahadharisha kuwa hali hiyo ya kutoelewana kibiashara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kuwa kikwazo katika ukuaji wa viwanda vya ndani na uboreshaji wa maisha ya raia.