Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, na kila mzazi hufurahia kuona watoto wake wanaishi katika mazingira mazuri yanayowawezesha kupata haki za msingi na kuwa raia wema katika kulitumikia taifa na kuleta maendeleo katika vizazi vijavyo.
Watoto wanatakiwa wajisikie salama wakiwa nyumbani, shuleni na kwenye jamii inayowazunguka. Lakini katika maeneo mengi ukatili dhidi ya watoto hufanyika na wakati mwingine kutoka kwa watu ambao wanawaona kila siku. Kwa watoto wengi suala la kufanyiwa ukatili linaonekana zaidi katika sura ya kifamilia.
Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu wakati akizindua Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto (2017 -2022), alisema kwa mujibu wa takwimu za jeshi la polisi vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vilivyoripotiwa 2015 vilifikia 22,876 kati ya hivyo vitendo vya ubakaji vilikuwa 3,444 , shambulio , kujeruhi na matusi vilikuwa 14, 561.
Suala ukatili wa dhidi ya watoto linatokea kila mahali kwa sura tofauti tofauti kulingana na mazingira anayoishi mtoto. Hata kwenye nchi ambazo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo bado wanakabiliwa na tatizo hili.
Ripoti iliyotolea hivi karibuni na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF-2017) inathibitisha dhana hiyo na kueleza kuwa watoto wanakutana na ukatili katika hatua zote za ukuaji wao katika mazingira wanayoishi,
“Mateso yanayohusisha watoto duniani kote yanasikitisha” anasema Mkurugenzi wa UNICEF Kitengo cha Ulinzi wa Watoto, Cornelius Williams. “ watoto wanapigwa usoni, wasichana na wavulana wanalazimishwa kufanya ngono; vijana wanauwa katika jamii zao- ukatili wa watoto hauvumiliki”.
“Robo tatu ya watoto walio na umri kati ya miaka 2 hadi 4 duniani kote ambao wanafikia milioni 300 wanakumbana na ukatili unaodhaniwa ni kuwafunza nidhamu kutoka kwa wazazi au watu wanaowalea wakiwa nyumbani” inaeleza ripoti hiyo,
“Watoto milioni 250 walio katika umri wa miaka 6 hadi 10 wanakumbana na adhabu za kupigwa. Watoto wengine wanaathirika kwa namna moja au nyingine kwa ukatili unaofanyika nyumbani. Duniani, Mtoto 1 kati ya 4 ambao ni sawa na watoto milioni 176 walio chini ya miaka 5 wanaishi na wanawake ambao ni waathirika wa vitendo vya ukatili walivyofanyiwa na waume zao”.
Ukatili pia unatokea maeneo ambayo watoto wanakusanyika na kujifunza zikiwemo shule na katika viwanja vya michezo.
Ripoti hiyo inathibitisha kuwa, “mwaka 2016 pekee, matukio 500 ya vitisho na kushambuliwa kwa watoto yaliripotiwa katika nchi 18 zilizoathiriwa na mapigano ya ndani. Watoto wanaohudhuria shule katika nchi ambazo hazina machafuko wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili”,
“Katika nchi 28 zenye data, wasichana 9 katika 10 ambao waliripoti kulazimishwa kufanya ngono kwa mara ya kwanza walisema walifanyiwa vitendo hivyo na watu walio karibu nao”.
watoto wakiponda mawe
Changamoto wanazokutana nazo watoto nchini Tanzania
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia Ripoti ya Haki za Binadamu 2016 kimebaini changamoto lukuki ambazo zinadumaza ustawi wa watoto nchini Tanzania. Changamoto hizo ni pamoja na:
1. Kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto ambapo vitendo zaidi ya 2, 571 vya ubakaji na ulawiti vimeripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.
2. Vitendo vya Ukatili wa kingono kufanywa na watu wa karibu kwa watoto; asilimia 49 ya vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vimeripotiwa kutekelezwa na ndugu wa karibu kwa watoto
3. Kuendelea kushamiri kwa ndoa za utotoni; watoto wawili (2) kati ya watano (5) huolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18.
4. Mimba za utotoni/mashuleni: Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) imeitaja Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa mimba za utotoni barani Afrika.
5. Vitendo vya kikatili na mateso dhidi ya watoto: Vitendo vya watoto kuunguzwa kwa moto, kupigwa hadi kuumizwa hata kujeruhiwa kwa visu au mapanga vimezidi kuripotiwa kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto jamii inashauriwa kujitathmini na kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wote ili wafikie ndoto za maisha yao.
Waziri mwenye dhamana Ummy Mwalimu amesema ukatili dhidi ya watoto unafanywa majumbani na shule hivyo kila shule ya msingi na sekondari ziundwe timu za ulinzi pamoja na kila kata kuwa na timu ya ulinzi.
Ripoti hiyo ya UNICEF inaeleza kuwa kwasababu yoyote ukatili wa kupigwa au wa kisaikolojia unamuachia mtoto kovu, na kumtengenezea mtazamo hasi dhidi ya familia na mahusiano na watu wengine katika jamii.
Ni vizuri kwa Watanzania kwa ujumla kutambua umuhimu wa kuzingatia haki za mtoto kwa kutowaficha wahalifu wa vitendo vya kikatili dhidi ya watoto hata kama ni ndugu wa karibu sana na badala yake kuwaibua na kuacha sheria kuchukua mkondo wake.
Pia ni vyema kwa vyombo vya usimamizi wa sheria ikijumuisha Jeshi la Polisi na Mahakama kuzingatia ustawi wa watoto wakati wa maamuzi na usimamizi wa haki. Na Serikali kufanyia marekebisho sheria zote zinazokandamiza ustawi wa watoto ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu msichana kuolewa akiwa na umri chini ya miaka 18.