Gesi kutomaliza matumizi ya mkaa Tanzania

Jamii Africa

KASI ya kukatwa kwa misitu kwa ajili ya kupata mkaa na kuni, huenda isipungue kama “inavyohubiriwa.”

Imebainika kuwa hata kupatikana kwa kwa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali, yakiwemo ya nyumbani, hakutakomesha matumizi makubwa ya mkaa nchini Tanzania.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonesha kwamba, hali hiyo itaendelea kushuhudia maelfu ya ekari za misitu zikiteketea ikiwa mipango madhubuti na endelevu haitakuwepo.

Tanuri likiwa limeandaliwa tayari kwa kuchoma mkaa.

Lubera Mato, mtaalamu wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, anasisitiza umuhimu wa kuweka mipango endelevu katika uzalishaji na biashara ya mkaa kwa ujumla ili kuilinda misitu ya Tanzania badala ya kuharamisha biashara hiyo.

“Mkaa (maarufu kama Biomass) ni nishati inayotegemewa na wananchi wengi hasa wa mijini, lazima tutafute njia mbadala ya kufanya biashara ya mkaa kuwa endelevu badala ya kuipiga marufuku,” Mato ameieleza FikraPevu.

Ingawa gesi asilia inaonekana kuwa nishati mbadala na rafiki wa mazingira, lakini wanaharakati wengine wa uchumi na maendeleo wanaona kwamba kuipiga marufuku ni kuwafanya Watanzania wanaoishi kwa kutegemea biashara hiyo kuendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini.

Serikali inabariki kukata misitu

 

“Ni ajira kubwa, mijini na vijijini… serikali inakusanya ushuru na wapo wafanyabiashara wenye leseni, huwezi kuiharamisha biashara ambayo wapo watu wanaitegemea kuendeshea maisha,” anasema Juda Lambert, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam.

FikraPevu inafahamu kuwa, inakadiriwa kwamba, Tanzania inapoteza wastani wa ekari 130,000 hadi 500,000 za misitu kila mwaka kutokana na uchomaji mkaa na uharibifu mwingine wa mazingira huku Shs. 11 bilioni zikipotea kila mwaka kwa matumizi yasiyo sahihi ya misitu.

Tanzania ina hekta milioni 35 za misitu, lakini milioni 13 kati ya hizo zimetengwa na serikali kwa ajili ya hifadhi za taifa.

“Tumeshauri kwamba, badala ya kukomesha biashara ya mkaa, ni vizuri kuihalalisha kwa kuweka mazingira bora na endelevu ya uvunaji wa misitu ili kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira,” Bwana Siang’a, ofisa kutoka Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), aliiambia FikraPevu.

Siang’a anaamini kwamba, ujio wa gesi hiyo inayochimbwa kusini mwa Tanzania umezingirwa na siasa zaidi kuliko uhalisia, huku akionya kwamba watakaonufaika ni watu wachache wenye fedha.

Anasema kwa miaka mingi wanamazingira wameshauri njia mbalimbali za nishati mbadala, ikiwemo matumizi ya umeme unaotokana na kinyesi cha binadamu, lakini serikali haijawahi kulitilia maanani suala hilo.

“Ni kweli gesi ipo, lakini uhalisia wa matumizi yake pengine wanaweza kuuona wajukuu zetu. Siasa ndiyo inayokwamisha mambo mengi na mazuri.

Hata Rwanda wanatushinda?

 

Ujenzi wa mtambo wa hewa-kani (biogas).

“Fikiria Rwanda wanatumia nishati inayotokana na kinyesi cha binadamu, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alipokwenda kule wakati fulani akashangaa na kutamani teknolojia hiyo ije huku, lakini akaambiwa wataalamu waliotengeneza ni Watanzania … aliporudi hakuna kilichoendelea mpaka ameondoka madarakani,” anasema.

Aidha, aliiambia FikraPevu kwamba, gesi hiyo ya kinyesi cha binadamu (biogas) inaweza kupatikana kwa wingi nchini Tanzania katika magereza na hata shule mbalimbali, lakini serikali inakosa uthubutu kutokana na mambo mengi kuendeshwa kisiasa.

Kwa hiyo, alisema, kupatikana kwa gesi asilia hakuwezi kuwa suluhu ya kukomesha biashara ya mkaa, ambayo nayo ina nafasi yake kiuchumi isipokuwa inahitaji kuwekewa mazingira mazuri zaidi ili isiwe adui wa mazingira.

Mkaa bado upo sana

Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Tanzania Demographic and Health unaeleza kwamba kuni na mkaa ni nishati inayotumiwa na asilimia 94.6 ya Watanzania kwa ajili ya mapishi.

Benki ya Dunia inaeleza kwamba, biashara ya mkaa nchini Tanzania inaingiza kiasi cha dola za Marekani 650 milioni (takriban Sh. 1.3 trilioni).

Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Felician Kilahama, aliiambia FikraPevu kuwa, mazingira yanaharibiwa sana kutokana na ukataji wa miti kwa mkaa na kuni, hivyo kushauri serikali itafute njia nzuri ya kukabiliana na hali hiyo.

“Mradi wa gesi asilia ni mkombozi wa mazingira na Watanzania kwa ujumla, lakini lazima iwepo mipango mahsusi ya kuhakikisha wananchi wananufaika na nishati hiyo.

“Kama ikiwezekana, basi watumiaji wa mkaa wapewe ruzuku ili kuangalia nishati nyingine mbadala kuokoa misitu yetu,” alisema.

Katika mojawapo ya tafiti zake, Kilahama anasema, misitu inafyekwa kwa kiasi kikubwa ili kuwawezesha wananchi walio katika biashara ya mkaa na kuni kuendesha maisha yao.

“Tani tano za miti zikichomwa zinatoa tani moja ya mkaa, sasa kama matumizi ya jiji kama Dar es Salaam ni magunia 50,000 kwa siku, maana yake miti mingi hapo imeteketea,” anasema.

Umoja wa Mataifa watushtua

Baadhi ya mitambo ya kuchakata gesi katika kituo cha Madimba mkoani Mtwara.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira (UNEP) linasema kwamba hekta milioni 107 za misitu zimepungua kwa asilimi 9 na kufikia hekta milioni 98 katika kipindi cha kati ya mwaka 1990 na 2000, lakini zikapungua tena kwa asilimia 13 hadi kufikia hekta milioni 85 mwaka 2010 kutokana na kufyekwa kwa misitu.

Japokuwa Tanzania bado inaongoza kwa kuwa na eneo kubwa la misitu, lakini FikraPevu inafahamu kwamba, imepoteza hekta milioni 15 ikifuatiwa na Kenya iliyopoteza asilimia 18 ya misitu yake na Burundi imepoteza hekta 117,000.

Kwa mujibu wa UNEP, Afrika inazalisha tani 30.6 milioni za mkaa (takwimu za mwaka 2012),ukiwa na thamani ya kati ya dola 6.1 bilioni na dola 24.5 bilioni kwa mwaka.

Nchini Kenya, mkaa unatumiwa na asilimia 82 ya wakazi wa mijini wakati asilimia 34 wanaoishi vijijini wanatumia nishati hiyo, ambapo wastani wa matumizi hayo ni kati ya tani milioni moja na milioni 1.6 kwa wananchi milioni 40.

Kukabiliana na janga hili la uharibifu wa mazingira, gesi asilia inaweza kuwa mkombozi ikiwa mikakati madubuti itawekwa na kutekelezwa ipasavyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *