Wakazi wa Songea wakosa huduma ya Vipimo kufuatia darubini kutumia mwanga wa jua

Mariam Mkumbaru

Wakazi wa kijiji cha Ifinga katika kata ya Ifinga wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma, wanakosa huduma ya vipimo vya maabara kwa kutokana na Darubini kutumia mwanga wa jua na kipindi hiki cha mvua kifaa hicho hakiwezi kufanya kazi.

Tobias Milinga (35) ni mtaalamu wa maabara katika zahanati ya Ifinga, anasema kuwa kipindi cha mvua kifaa hicho hakiwezi kufanyakazi kabisa, hivyo wagonjwa wanapatia dawa kwa jinsi anavyosema ugonjwa wake na kwa kumuangalia kwa macho.

"Nimeanza kazi ya maabara kwa muda wa miaka 18, katika zahanati mbalimbali lakini sijawahi kuona Darubini inatumia mwanga wa jua kama kupima magonjwa mbalimbali, na kipindi cha mvua kama hiki huwezi kuitumia Darubini hii,"alisema Milinga.

Darubini

Milinga alisema kuwa, tatizo kubwa katika zahanati hiyo, ni kutokuwa na umeme wa solar ambao ungeweza kutumika katika Darubini hiy0, pia kunatatizo la maji, kifaa cha kumsafisha mjamzito mimba ikiharibika hakuna, kifaa cha kumsafisha mtoto akinywa maji machafu baada ya kuzaliwa hakuna pamoja na madawa ya kutibu magonjwa mbalimbali hakuna.

Milinga alisema kuwa, pia kuna tatizo la uhaba wa wahudumu katika zahanti hii, kwa sasa tupo watumishi wawili tu, akiwemo nesi mmoja, kwa sababu hiyo  inanilazimu kuwaona wagonjwa pamoja na kuwapima magonjwa mbalimbali kila siku.

Aidha alisema kuwa, kutokana na tatizo la uhaba wa wahudumu kwa muda mrefu, mfanya usafi wa zahanati hii Benjamin Kalunguyeye (55) imemlazimu kuanza kutoa huduma mbalimbali kwa wanakijiji kama tabibu.

"Nimeripoti katika zahanati hii mwezi Agosti mwaka jana 2011, nikamkuta Kalunguyeye anatoa huduma akiwa peke yake baada wa wahudumu kukimbilia mjini na kuacha zahanati bila ya mhudumu,"alisema Milinga.

Kwa upande wake Kalunguyeye alisema kuwa, kazi ya kuwatibu wanaifinga amaianza mwaka 1990, kwa sasa anamiaka 22 anatoa huduma katika zahanati hiyo kama, kungoa meno, kuzalisha, kuchoma sindano, kutoa chanjo kwa watoto wadogo, kupima wajawazito, kusafisha vidonda na kupima magonjwa ya maabukizi kama Gono, Kaswende na Kisonono.

"Elimu yangu ni darasa la saba lakini naipenda kazi ya utabibu na naifanya vema kama nimesomea katika chuo cha utabibu, kitu kikubwa kilichonisukuma kujua kazi hii, nikufuatia wahudumu kukimbia zahanati hii na kuniachia mimi kama mfanyausafi mara kwa mara, huku nikiwaona wanakijiji wenzangu wakipoteza maisha kwa kukosa huduma,"alisema Kalunguyeye.

Mwaka 1985, aliajiriwa na Kanisa kama mfanya usafi katika zahanati hiyo, hapo ndio akaanza kujifunza jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa mbalimbali kupitia kwa waganga na manesi waliowahi kufanya kazi katika zahanati hiyo.

Ilipofika mwaka 1989, hapo ndio akaanza kuibia ibia kutoa huduma mbalimbali kwa wanakijiji baada ya mganga na nesi kukimbia kwa visingizio kwamba kijiji cha Ifinga, hakuna maji safi, umeme, usafiri pamoja na mawasiliano ya simu.

Kwa upande wake Father Roja Haule wa Kanisa Katoliki Ifinga alisema kuwa, zahanati hiyo inamapungufu mengi yakiwemo la vifaa vya muhimu vya kutolea huduma, madawa, umeme, maji pamoja na wahudumu wa afya, kwa sasa kuna mtaalamu wa maabara mmoja na nesi mmoja na mfanya usafi ambaye anatoa huduma kwa uzoefu bila ya kusomea utabibu.

Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Songea Dokta Daniel Masawe, alikiri kuwepo wa kifaa cha kupima magonjwa mbalimbali kinachotumia mwanga wa jua, na kipindi cha mfua hakina uwezo wa kufanya kazi kabisa.

"Nafahamu uwepo wa darubini ya kupimia magonjwa mbalimbali inayotumia mwanga wa jua, tunajipanga kwa sasa kununua kifaa kingine kinachotumia umeme wa solar, ili kipindi cha mvua wagonjwa mbalimbali waweze kupata huduma ya kupimwa na kutambua kinachowasumbua hususan kipindi cha mvua kama sasa,"alisema Dokta Masawe.

Daniel-Masawe

Dokta Masawe alisema kuwa tatizo upungufu wa wahudumu wa afya sio la Ifinga tu, bali ni zahanati nyingi kwa Songea zinakabiliwa na changamoto hiyo ya wafanya usafi kutoa huduma ya afya bila ya kwenda kusomea katika chuo cha utabibu.

Aidha alisema kuwa, kijiji cha Ifinga kimempitisha Kalunguyeye kuwa mhudumu wa afya, katika kikao cha maendeleo ya kata na kumfutia uchangiaji wa maendeleo ya kijiji kama ujenzi wa shule, ununuzi wa madawati, ujenzi wa nyumba za walimu.

Rosyita Lugongo ni katibu wa afya Jimbo la Songea,ndiye anayesimamia utoaji wa huduma za afya na ubora wa majengo hayo ya zahanati 14 na hospitali ya peramiho zilizojengwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Songea.

Juhudi za kumtafuta Katibu wa Jimbo hilo, kujibu matatizo mbalimbali ya zahanati ya Ifinga, mpaka kupitia kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ruvuma Dokta. Malecela kwa kumpigia simu na kwenda kuongea ili niweze kumuhoji changamoto hizo, alikata kata kata kuona na mimi na kumwambia Dokta Malecela  hataki kuongea nami.

Zahanati ya Ifinga imejengwa mwaka 1982 na Kanisa Katoriki Jimbo la Songea, baada ya serikali kushindwa kujenga zahanati katika vijiji mbalimbali na Kanisa kuamua kujenga zahanati hizo ili kuweza kuwafikishia huduma za afya kwa ukaribu zaidi.

Wakati sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa, serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha afya ya uzazi ya wanawake na wanaume, watu wenye ulemavu na wazee. Pia anaendelea kueleza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya vinovyowavutia wanawake, wanaume na vijana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *