Wakulima Kisarawe wagoma kuchukua mbegu za muhogo

Jamii Africa
Shamba la mbegu Kisarawe

Bwana Shamba wa Kijiji cha Mhaga wilayani Kisarawe, David Shangali, akiwa pembeni ya shamba darasa la mihogo linaloangaliwa na uongozi wa kijiji hicho kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za Kibaha 026. Mbegu hizo zimekataliwa na wakulima.
 

WAKATI kiasi cha Dola za Marekani bilioni moja (takriban Shs. 2.1 trilioni) kimetengwa kuimarisha zao la muhogo nchini, wakulima wa Kijiji cha Mhaga, Kata ya Kibuta, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wamegoma kuchukua mbegu mpya za zao hilo wakidai zinawatia hasara, FikraPevu inaripoti.

Wakulima hao wamedai kwamba mbegu hiyo inayofahamika kwa jina la Kibaha 026/Mkuranga 1 siyo rafiki wa mazingira na zitawatia umaskini badala ya kuwanufaisha.

Mbegu hiyo ambayo ilibuniwa na Kituo cha Kilimo Kibaha baada ya utafiti wa miaka mitatu ulioigharimu serikali fedha nyingi inadaiwa kutumia gharama nyingi wakati wa palizi kwa kuwa inakaa shambani miezi 12 kabla ya kuvunwa, tofauti na aina nyingine ya mbegu.

Watafiti katika Kituo cha Kibaha walibuni mbegu hiyo katika jitihada za serikali za kupata mbegu bora na kinzani kwa magonjwa yanayoshambulia zao hilo.

Muhogo uliopatikana kutoka katika mbegu ya Kibaha 026 au Mkuranga 1 uliovunwa baada ya mwaka mmoja na miezi mitatu na kupata mvua ya kutosha. (Picha na. Sobo Aisi)

 

“Mbegu hii siyo mkombozi kwa wakulima, itatutia umaskini kwa kutumia gharama nyingi katika palizi, lakini pia mihogo inakuwa na mizizi mingi kutokana na kukaa muda mrefu ardhini,” walisema wakulima hao.

Januari 14, 2017 Serikali ya Tanzania ilitiliana saini na kampuni ya Tanzania Agricultural Export Processing Zone Limited and Epoch Agriculture (TAEPZ) kutoka China kwa lengo la kuimarisha zao hilo na kuongeza ubora na uzalishaji ili kusafirisha katika nchi hiyo ya Mashariki ya Mbali.

Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru, alisema huo ulikuwa wakati wa wakulima kunufaika na kilimo cha muhogo badala ya kulima kimazoea.

Asilimia 80 ya wakazi 10,146 wa Kata ya Kibuta wanajihusisha na kilimo, hususan mihogo, lakini kuikataa mbegu hiyo kunaonekana kuwarejesha kwenye changamoto za siku zote za kutumia mbegu za kubahatisha ambazo zinadaiwa hazistahimili magonjwa.

Wakulima hao wanasema, awali walikuwa wakitumia mbegu ijulikanayo kwa jina la Rasta ambayo iliwaletea mavuno mengi kabla ya kuathiriwa na ugonjwa wa batobato na michirizi ya kahawia.

Inaelezwa kwamba, baada ya mbegu ya rasta kuathiriwa na magonjwa wakulima walilazimika kutumia mbegu ya Kiroba au Enyimba ambayo bado imeonekana kuwa na changamoto katika upatikanaji wa soko kwani mihogo yake huwa michungu endapo itacheleweshwa kuvunwa.

Uzaaji wa mbegu ya rasta unadaiwa ulikuwa mzuri na kuwanufaisha wakulima, ambapo kwa ekari moja mkulima aliweza kuuza hadi shilingi milioni moja tofauti na Kibaha 026 ambayo wanapata shilingi 600,000 tu kwa ekari moja.

"Hii mbegu kwa ujumla haitufai, inatutia hasara ni afadhali waturudishie ile mbegu ya rasta," walisisitiza wakulima hao.

FikraPevu ilifika katika shamba darasa la mbegu za Kibaha 026 zinazoelezwa kuwa ni bora, lakini licha ya mbegu hizo kukataliwa na wakulima, shamba hilo lenye ukubwa wa ekari nne limetelekezwa na kugeuka pori.

Muhogo ambao haukupata mvua ya kutosha kama ilivyolalamikiwa na wakulima na kutolewa ufafanuzi na Bwana Shamba wa eneo hilo.

FikraPevu imefanikiwa pia kuona mihogo ambayo baadhi ya wakulima wameilalamikia kwa kuwa na pingili zenye mizizi, hali inayodumaza soko la zao hilo.

David Shangali ni Ofisa Ugani wa Kijiji cha Mhaga ambaye anasema kuna changamoto kubwa kuhusu mbegu hizo na kwa muda mrefu wakulima wamegoma kuzichukua.

Awali, Shangali alisema kwamba, mbegu hizo zitagawiwa kwa wakulima wote watakaozihitaji na kuorodhedha majina yao kwa uongozi wa kijiji na kwamba wangepatiwa mizigo mitatu yenye fito 30.

Lakini kwa mujibu wa wakulima hao, hata kama mbegu hiyo ingekuwa inafaa, kiasi hicho walichopanga kuwapatia ni kidogo na hakiwezi kutosheleza hata katika eneo lenye ukubwa wa robo eka.

Ofisa mmoja mwandamizi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kibaha ambacho kilibuni mbegu ya Kibaha 026 amekiri kukataliwa kwa mbegu hizo na wakulima na akasema hajui sababu ni nini.

"Ni kweli wakulima wamegoma kuzichukua ingawa hivi sasa nasikia wanakwenda mmoja mmoja, hatujui tatizo ni nini hasa," alisema ofisa huyo ambaye alisihi hifadhi ya jina lake.

Kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya hali ya hewa, wataalam wa kilimo wanashauri kulimwa kwa mazao yanayostahimili ukame kama mihogo na mtama ili kujihami na kujikinga na njaa kutokana na kukosekana kwa mvua kwa wakati.

Zao la muhogo hustawi zaidi maeneo yaliyopo umbali wa meta 0-1500 kutoka usawa wa bahari na maeneo ambayo hupata mvua za wastani wa milimeta 750- 1200 kwa mwaka.

Enyimba na Kibaha 026 ni miongoni mwa mbegu zilizothibitishwa na wataalam kuwa zinaweza kustahimili magonjwa kama batobato na matekenya au michirizi ya kahawia.

Aidha, wataalam hao wanashauri wakulima watumie mbegu inayoendana na aina ya udongo pamoja na hali ya hewa ya eneo husika.

Serikali imekuwa ikijitahidi kutafuta fursa za masoko kwa wakulima, yakiwemo ya nje ya nchi kama walivyofanya hivi karibuni baada ya kusaini makubaliano na kampuni kutoka China iliyoamua kuwekeza nchini kwa lengo la kusindika mazao yatokanayo na muhogo badala ya kusafirisha muhogo ghafi ambao huyanufaisha mataifa ya nje na kuikosesha serikali mapato.

“Lengo la serikali kuwa na uchumi wa viwanda linaanza kutimia, huu ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo cha biashara. Kutakuwa na shamba kubwa la mihogo, kutajengwa viwanda mbalimbali vya kuzalisha unga wa mihogo, makopa, chakula cha mifugo, sukari ya viwandani na mbolea.

 “Hii fursa tusiiache, kama mlikuwa mnalima mihogo kwa kiwango kidogo ongezeni mashamba kwa sababu soko la uhakika lipo, pia tunashauri mnunue hisa katika kampuni hii ili ikiwezekana tuimiliki kwa kiwango kikubwa,” alisema Dk. Meru.

Aliongeza kuwa mradi huo utasaidia wakulima wa mihogo kuongeza ufanisi na kuhakikisha wanapata mbegu bora ili kufikia kiwango kinachotakiwa katika kipindi cha miaka mitano ya majaribio, ambacho pia kitakuwa na mafunzo juu ya kilimo bora cha zao hilo na namna ya kusindika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye, aliwataka wakulima kugeukia kilimo cha muhogo kwa sababu wawekezaji hao wanahitaji tani milioni tano kwa mwaka.

“Takwimu zinaonyesha Tanzania tunazalisha tani milioni tano za mihogo mibichi kwa mwaka, kampuni ya TAEPZ inahitaji tani milioni 2.5 za muhogo mkavu (makopa), maana yake ikiwa mibichi kutoka shambani inakuwa na uzito mara mbili.

 “Tumeamua kuwaita wawekezaji kwa sababu tuliwahi kupewa fursa ya kusafirisha tumbaku na nyama kwenda China, lakini tulishindwa kutimiza vigezo kutokana na kila mmoja kusafirisha kwa namna yake bila kuzingatia ubora, naamini katika hili tutafanikiwa kutimiza malengo tuliyojiwekea,” alisema Simbeye.

Kwa sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza Afrika kuwa na uwekezaji mkubwa kutoka China ambapo kiasi cha Dola za Marekani 6.62 bilioni (takriban Shs. 13.24 trilioni) kimewekezwa nchini katika miradi mbalimbali.

China imeahidi kuwa, katika usafirishaji mihogo watahakikisha Tanzania inazipita Nigeria na Ghana ambazo ndizo zinazoongoza kwa kusafirisha zao hilo kwa sasa.

Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng alisema wameamua kuichagua Tanzania katika mradi huo kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba na wananchi wengi kujishughulisha na kilimo cha mihogo lakini hawana soko la uhakika.

“Tanzania kuna fursa nyingi za kilimo, katika awamu ya kwanza ya mradi huu tutaanzisha kiwanda za kusindika mihongo katika mikoa mitatu ambayo ni Lindi, Pwani na Mtwara, ingawa baadaye tutaongeza mikoa mingine mradi utakapoonyesha mafanikio.

“Tuna imani na kasi ya awamu hii na ndiyo maana tumekubali kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu serikali itatusaidia kuhakikisha mradi unafanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Feng.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *