Taarifa ya uchunguzI wa vifo vya wananchi waliouawa mikononi mwa Polisi huko Tarime inadaiwa kuonesha kuwa marehemu wote wanne walipigwa risasi kutokea nyuma ikiashiria kwamba walikuwa wamewapa migongo polisi. Kwa mujibu wa sehemu ya taarifa hiyo ambayo ilitolewa kwenye mtandao dada wa FikraPevu wa JamiiForums.com jana jioni na mmoja wa wataalamu waliouhudhuria uchunguzI huo Bw. Grayson M. Nyakarungu ambaye aliwakilisha familia katika uchunguzI huo.
UchunguzI huo ulifanywa na Dk. Makata kutoka Wizara ya Afya, kitengo cha Dharura na matukio tata. Pamoja na uwakilishi wa familia, jeshi la Polisi na hospitali ya wilaya ya Tarime nao waliwakilishwa. Kwa mujibu wa Bw. Nyakarungu kati ya miili mitano ya watu waliouawa katika tukio hilo la Mei 19 ni miili minne ndiyo ilifanyiwa uchunguzI huku mwili mmoja ukiwa umeshazikwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa Bw. Nyakarungu uchunguzI huo ulianza kufanyika kuanzia kati ya saa nne na nusu asubuhi na saa kumi na moja jioni mara baada ya wanafamilia kutambua miili ya ndugu zao. UchunguzI wa kwanza ulikuwa wa mwili wa Emmanuel Magige risasi inaonekana kuingia tokea upande wa juu kushota wa nyonga (kiuno) na kutokea juu karibu na uti wa mgongo huku risasi hiyo ikiwa imepasua mishipa ya damu na kuvunjavunja vunja mfupa wa kiuno na kusababisha damu nyingi ambavyo vilisababisha kifo.
Pamoja na jeraha hilo la risasi ripoti hiyo inaonesha kuwa kulikuwa na jeraha chini tu ambapo risasi ilitokea na linaonekana kama limesababishwa na ncha ya kitu kikali. “hii ilileta hisia tofauti, polisi walihisi kuwa aliangukia jiwe au kijiti kilichomchoma, kwa hili tulibishana na tukaamua hakuna jibu la nini kilichoma, ila mimi nilihisi na kusimamia kuwa alichomwa na singe ya bunduki, na ndipo niliomba nguo zake zitafutwe ili tuzichunguze na tubaini ukweli, hata hivyo hazikupatikana.” amesema Bw. Nyakarungu.
Kwenye mwili wa Chacha Ngoka risasi inaonekana kuingia kupitia chini ya bega ba kutokea mbele kulia chini kidogo ya ziwa lake. Viungo vya ndani vilivyojeruhiwa ni pamoja na kupasuliwa kwa maini na damu kuonekana kuganda katika mrija wa koo vitu ambavyo vilisababisha kifo. Mwili wa Chawali Boke unaonesha kuwa risasi iliingia kupitia kisogoni kama sentimeta 8 kutoka sikio la kushoto na kutokea kwenye paji la uso “pembeni kidogo”. Kilichosababisha kifo ni kuharibiwa kwa ubongo na risasi hiyo.
Katika mwili wa Mwikwabe Marwa Mwita taarifa hiyo ya kitaalamu inasema kuwa risasi pia iliingilia upande wa juu wa kiuno kutokea nyuma lakini risasi haikutoka na kubakia ndani ya mwili. Risasi hiyo ilipasua mishipa ya damu ya kwenda miguuni, misuli ya jirani, pamoja na kuvunja mfupa wa nyonga na uzazi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo kipande cha risasi kilionekana kikiwa ndani kwenye msuli mmojawapo.
Kwa maoni yake ambayo hadi tunachapisha habari hii hayajaonekana kuungwa mkono na wengine walioshiriki uchunguzI huo Bw. Nyakarungu ni kuwa vifo vya watu hao havikutokea katika mazingira ambayo Polisi inaweza kudai kuwa ilikuwa inatishiwa nao na hivyo walikuwa wanajihami bali vilitokea wakati watu hao wakiwa wamewapa mgongo polisi “wakikimbia”.
Bw. Nyakarungu anaandika na kusema kwa uhakika kuwa “Polisi walikusudia kuua na sio kudhibiti watu waliowaita wavamizi, kwani kwa mujibu wa force law, hawakutakiwa kupiga risasi sehemu yoyote tofauti na miguuni” na kuongezea kuwa “waliwapiga risasi watu waliokuwa wakikimbia kutoka eneo hilo, kwani risasi zote zimepenya kwa upande wa nyuma wa mwili na zikatokea upande wa mbele wa mwili.”
Endapo madai ya ripoti hiyo yatakuwa ndivyo yalivyo kama inavyodaiwa na Bw. Nyakarungu ni wazi kuwa hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Watanzania kuoneshwa ukatili wa jeshi la Polisi dhidi ya raia kwa kuwapiga watu ambao hawana silaha tena waliokuwa wakikimbia. Hili litasababisha kwa maoni ya wanaharakati wa haki za binadamu kuhoji uwezo wa jeshi la polisi kuzuia vurugu bila kulazimika kutumia risasi za moto na kusababisha mauaji. Zaidi ya yote linahoji kwa uzito zaidi kama viongozi wa sasa jeshi la Polisi wanastahili kuendelea na nafasi zao hasa baada ya mlolongo wa matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu chini ya uongozi wao ikiwemo yale matukio ya mauaji ya Arusha Januari 5 mwaka huu.
Hadi hivi sasa haijajulikana ni kwanini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora haijaanza uchunguzI mara moja moja au hata kuonekana kutaka kufuatilia. Inahisiwa kuwa yawezekana tume hiyo inasubiri kuombwa au kuagizwa ndio ifanye kazi yake badala ya kufanya kazi mara matukio kama haya yanapotokea mara moja. Tume hii ambayo imempata Katibu wake mpya hivi karibuni imekuwa ikitoa maelezo tu ya kile ambacho watu wengi tayari wanakijua lakini haijawahi kuwa na uthubutu wa kuagiza watu (hasa viongozi wa juu) kuachishwa kazi kwa kuvunja haki za binadamu. Haijajulikana kama ripoti hii itafanya tume hiyo kuchukua msimamo wa kutetea haki za Watanzania waliouawa mikononi mwa Polisi.
Wakati tukio lenyewe la mauaji likiendelea kuzua utata, siku ya Jumatatu usiku jeshi la Polisi linatuhumiwa kuchukua miili hiyo baada ya uchunguzI na kulazimisha kuipeleka kwenye familia ilhali kulikuwa na makubaliano kati ya familia, jeshi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (ambao ndio wanaunda serikali ya kata) kuwa miili ingeondoka siku ya Jumanne kuelekea kwenye uwanja wa sabasaba kwa ajili ya ibada ya kuiaga.
Hata hivyo familia hazikuwa tayari kupokea miili kwa namna hiyo na matokeo yake katika maeneo kadhaa majeneza yaliyoletwa na polisi yakiwa na miili yaliachwa barabarani (angalia picha) baada ya familia kutokuafiki jambo hilo. Kitendo hicho kimechukuliwa na baadhi ya watu kama uvunjwaji mkubwa wa utu wa binadamu na kutojali mila, desturi na imani na kama hakukuwa na sababu ya viongozi wa polisi kuachishwa kazi kwa mauaji basi kwa kitendo cha kukufuru miili (desecration of the dead) wanapaswa kuomba radhi mara moja na kuwajibishwa.
Pamoja na hilo kulikuwa na taarifa vile vile ya waandishi wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Nipashe wamekamatwa wakidaiwa kuwashawishi ndugu wa marehemu kugoma kuchukua miili toka mikononi mwa polisi.
Mwandishi Maalum Tarime
Miaka 50 baada ya Uhuru askari polisi bado wanaua raia wake bila sababu za msingi.
Ni vurugu hizi kwa kweli; tutafika kweli?
sasa leo yametokea urambo hatutafika kabisa sijui kesho itakua wapi na sijui wakina Ocampo wapo wapi?
Hayakuanza leo haya!
Waliuawa watu wasio na siraha Mwembechai na majeruhi mtoto mdogo alifungwa pingu kitandani akiwa hospitali kapooza HAPAKUTOKEA HATA KAULI ZA WANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU
Walikuwa majambazi tu ni haki yao kufa kwa staili hiyo, kama wangepigiwa risasi majumbani kwao au barabarani hapo jeshi lingewajibika. Uvamizi kwenye eneo lisilo lako tena kwa mabavu lazima nguvu itatumika kukuondoa na pengine RISASI za moto.
Siasa ndo inataka kubadilisha ukweli kwa maslahi yao, Uhalifu upo pale pale hata kikiwapo chama kingine madarakani kitasimamia haya haya.