“Ukimkomboa mwanamke umeikomboa jamii yote” ni usemi ambao umezoeleka hasa kwa wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto ambao huamini kuwa mwanamke ana nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii ikiwa atapewa nafasi ya kutekeleza majukumu kwa haki na usawa.
Kabla haujamzungumzia mwanamke lazima uanze na mtoto wa kike ambaye anatakiwa aandaliwe mazingira mazuri ya malezi na ukuaji yatakayomtengenezea mstakabali mzuri wa maisha ya kuwa mwanamke anayeheshimika na jamii. Ikiwa jamii haitamlinda msichana na kumpatia staili zake muhimu hataweza kufika hatua ya kujitambua na kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.
Tumeshuhudia jinsi wasichana wengi nchini wanavyokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambayo ni matokeo ya mkanganyiko wa maadili na mabadiliko ya mfumo wa maisha miongoni mwa watu wengi.
Mabadiliko hayo yamewaathiri wasichana na kuonekana kuwa ni wakosaji na watu waliotengwa na jamii zao, lakini jamii isijue kuwa muonekano wa jamii fulani unatengenezwa na wanajamii wenyewe. Tatizo ambalo linaibua mjjadala mbalimbali ni mimba za utotoni ambazo wasichana wengi wanazipata wakiwa katika umri mdogo ambapo kitaalamu zina madhara makubwa kwa sababu mtoto aliye chini ya umri 18 hawezi kuhimili mabadiliko ya kiafya yanayotokea wakati wa ujauzito.
Mimba za utotoni ni matokeo ya sababu mbalimbali, ukosefu wa elimu ya uzazi katika maeneo mengi ya nchi hasa mashuleni, wasichana kutokujua mabadiliko wanayopitia na jinsi ya kujikinga ili wasitumbukie katika mimba. Elimu hii sio dhamana ya serikali pekee bali inaanzia ngazi ya familia. Lakini kutokana na tamaduni za jamii mbalimbali ni vigumu kwa wazazi kuwafundisha watoto masuala ya uzazi na wasichana kukosa muelekeo wa kuufuata hasa wanapokutana na mabadiliko katika miili yao.
Mtazamo hasi walionao baadhi ya watu kuwa thamani ya msichana ni kuolewa na kuwa mama wa kulea watoto pia imezidisha tatizo. Mitazamo hii huwakatisha tamaa wasichana kutokana na kufuata desturi za ubaguzi ambazo zinalenga kumdidimiza mtoto wa kike katika kufaidika na rasilimali za jamii ikiwemo kupata elimu bora.
Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani (2016) unaitaja Tanzania kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa za utotoni na mimba kwa asilimia 28, ambapo kila mwaka wasichana 8,000 hupata mimba na kukatisha masomo.
Hali si salama kwa wasichana wengi ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha kwa sababu ya mimba za utotoni na kujifungua nyumbani. Wasichana hawa hulazimika kujifungulia nyumbani ili kukwepa aibu na mkono wa dola ambao huwatia hatiani na kuwalazimisha kukatisha masomo yao.
Licha ya juhudi mbalimbali za kudhibiti mimba za utotoni, vifo vingi vimekuwa vikiripotiwa maeneo mbalimbali nchini na kuwafanya wasichana kupoteza ndoto za kufanikiwa. Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) linaeleza kuwa vifo vya uzazi vinavyohusiana na mimba katika umri mdogo vinatokea sana katika umri kati ya miaka 15 na 19, hivyo kuwa na vifo vya wasichana 50,000 kila mwaka duniani kote.
Tanzania kwa kushirikiana na Asasi za kiraia katika kipindi cha miaka 6 iliyopita imefanikiwa kupunguza tatizo la mimba za utotoni kwa asilimia 13. Japokuwa wakati huu msichana 1 kati ya 6 walio katika umri wa miaka 15 na 19 ameolewa. Lakini maeneo ya vijijini wasichana wadogo wa umri wa miaka 12 wameolewa.
Ripoti ya utafiti wa shirika la watoto duniani (UNICEF) katika kufahamu ukweli wa mimba za utototni ilikutana na msichana Christina mwenye umri wa miaka 14 ambaye aliolewa akiwa na umri wa miaka 12. Christina alisema anaishi katika nyumba ndogo ya matope na mmewe John na mama yake wa kambo.
Christina alisema “nataka kuwa na watoto wa watatu,lakini nasubiri mpaka nifike umri wa miaka 18 au 20. Mama yangu wa kambo anahitaji niwe na watoto 6 lakini nitawasomeshaje, na kuzaaa watoto wote sita?”.
Bado wasichana wengi wako katika hatari ya kupata mimba za utotoni hasa maeneo ya vijijini ambako hawafikiwi na elimu ya kutosha. Lakini waliopata nafasi ya kwenda shule bado wanakabiliwa na changamoto za umaskini na mazingira yasiyoridhisha ya kusomea, wengine huamua kukatisha masomo na kujiingiza katika biashara ya ngono kwa kushawishiwa na wanaume wasio na utu na malezi bora ya familia.
Takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za mwaka 2010 zinaonyesha katika shule za sekondari wanafunzi waliokatisha masomo walikuwa ni 66,069 huku mimba na utoro ikiwa ni sababu kuu, pia katika shule za msingi walikuwa wanafunzi 76,246 na waliofukuzwa kwa sababu ya mimba ni 1,056.
Ikiwa tunahitaji kujenga mstakabali mzuri wa mwanamke tunatakiwa tuwekeze nguvu kubwa kuwatengenezea wasichana wadogo mazingira mazuri ya ukuaji yanayoambatana na elimu bora ambayo itawafanya wajitambue na kupinga vitendo vya ubaguzi na ukandamizaji dhidi ya wanawake na watoto.
Tukibadilika na kujenga jamii inayoheshimu haki na usawa wa kijinsia Taifa letu litapiga hatua kubwa ya maendeleo, dhamana ya nchi iko mikononi mwa wanawake tuwape nafasi na kuzidi kukubali michango wanayoitoa. Matatizo wanayowapata watoto wa kike yanaliathiri taifa lote, tuungane na kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la mimba za utotoni ili kuthamini maisha ya kila raia bila kujali nafasi ya mtu katika jamii.