Wanawake watakiwa kujitokeza kutibiwa ugonjwa wa fistula

Gordon Kalulunga

WITO umetolewa kwa wanawake wanaosumbuliwa na tatizo la kutokwa na haja ndogo mfululizo na haja kubwa katika sehemu zao za siri kujitokeza kupata matibabu yanayotolewa bure katika hospitali teule ya wilaya ya Mbeya Mbalizi-Ifisi iliyopo wilaya ya Mbeya Vijijini.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Msafiri Kimaro na Ofisa Muuguzi Mkuu Roda Kasongwa walisema kuwa hospitali hiyo inawatibu wagonjwa wenye matatizo hayo bila kuwatoza gharama zozote.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo alisema ugonjwa huo umewaathiri zaidi mabinti wanaopata mimba chini ya miaka 20 na baadhi ya wanawake wanaojifungua katika uzao wao wa kwanza.

‘’Wanaoathirika zaidi ni wale wanaopata mimba wakiwa chini ya umri wa miaka 20 na baadhi wanaojifungua katika uzao wao wa kwanza hasa wanaotoka vijijini ambako huduma za Afya ziko mbali nao’’

‘’Mwaka jana wanawake watano walijitokeza na kubainika kuwa walikuwa na Fistula kutoka maeneo ya vijijini ambapo wawili walitoka eneo la Kamsamba wilayani Mbozi, Mmoja alitoka mjini Tunduma wilayani Mbozi na wawili walitoka eneo la Ikukwa Mbeya Vijijini’’ alisema Kimaro.

Aidha alifafanua kuwa, ugonjwa huo katika wilaya ya Mbeya Vijijini upo ambapo kwa mara ya kwanza katika hospitali hiyo walifanikiwa kuwatibu wagonjwa wawili ambao mmoja alipata ugonjwa huo mwaka 1961 na mwingine alipata tatizo hilo mwaka 1978.

Naye Ofisa Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo Rhoda Kasongwa ambaye ana uzoefu wa miaka 40 katika tasinia ya afya hapa nchini, alifafanua kuwa wanawake wengi hawajitokezi kutibiwa kitaalam baadhi wakidhani kuwa kuna gharama za matibabu na wengine ni kuwa mbali na huduma za afya kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.

‘’Katika hospitali yetu tunatoa matibabu ya fistula bure kwa wanawake wenye matatizo ya kuvuja mkonjo na mtaalam wa tatizo hilo ni Doctor Kimaro na kuna wanawake ambao matatizo yao yalikuwa makubwa zaidi tuliwapeleka hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam kwa gharama za hospitali’’

‘’Wale wanaofanikiwa kutibiwa tatizo hilo tunawapatia pia nauli za kuwafikisha mpaka nyumbani kwao ama maeneo wanayoishi na hiyo yote inatokana na kutambua umuhimu wa kuwahudumia wanawake hapa nchini ambao ni nguzo za familia’’ alisema Kasongwa.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa hospitali hiyo alitoa angalizo kuwa wagonjwa wanaotibiwa fistula wanapaswa wanapopata ujauzito kuwa karibu na Hospitali kwasababu wanatakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na kama wakijifungua kwa njia ya kawaida tatizo la fistula linaweza kujirudia kutokana na mgandamizo unaojitokeza wakati wa kujifungua.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *