CHAMA cha Madaktari Kanda ya Ziwa (MAT), kimemshutumuk Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya kwa kauli yake waliyoiita ya kejeli kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (NMH), waliogoma, na kusema kiongozi huyo aache kuwatisha.
Kadhalika, MAT kimeionya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuachana na hulka ‘mbovu’ ya kuwatisha na kutowalipa mishahara kwa wakati madaktari na wataalamu wengine, badala yake iboreshe mishahara na huduma za afya kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Mwanza na mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Kanda ya Ziwa Victoria, Dk. Rodrick Kabangila wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao na madaktari, kilichofanyika hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini hapa.
Dk. Kabangila alisema, Madaktari wamekasirishwa sana na kauli mbaya ya Waziri Nkya aliyoitoa hivi karibuni kuhusiana na mgomo wa madaktari wa Muhimbili, na kwamba kiongozi huyo anatakiwa aache kabisa kuwakejeri wataalamu.
“Huyu Naibu Waziri ametudharirisha sana madaktari. Anasema eti kazi ya madaktari ni taaluma tu na wapo chini ya Serikali.
“Yupo pia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera na yeye ametukejeli sana madaktari na manesi. Anasema eti sisi madaktari tunachangia sana vifo vya wananchi…hizi ni dharau za kupitiliza”, alisema.
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Dk. Kibangila ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Taznania, alisema MAT Kanda ya Ziwa itaendelea kuunga mkono maamuzi ya vikao vyote vinavyoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema, chama cha Madaktari Kanda hiyo kipo tayari kutekeleza maamuzi yatakayofanywa na MAT taifa, na kwamba hawatarudi nyuma kutekeleza kila hatua itakayofikiwa kupitia ngazi ya taifa.
“Chama cha Madaktari Kanda ya Ziwa, tunaunga mkono kila hatua na hatua zitakazofanywa na MAT taifa, na tupo nao pamoja kwa kila jambo”, alisisitiza mwenyekiti huyo wa MAT Kanda ya Ziwa.
Maazimio mengine waliitaka Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha inaboresha zaidi maslahi na mishahara ya wataalamu hao, ikiwa nipamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, dawa na mambo mengine ili kuondoa wimbi la Watanzania kukimbilia nchini India kupata matibabu.
Alisema, Seriakli iangalie tiba mbadala na kusaidia wananchi, itoe stahiki za madaktari na marupurupu yao bila kinyongo, mishahara iangalie ugumu wa kazi wa madaktari.
Awali, baadhi ya madaktari waliishambulia Serikali kwa madai kwamba, ni aibu kupapandisha posho za Wabunge na kushindwa kuwalipa mishahara midogo madaktari ambao kazi zao ni ngumu zaidi.
“Kwa nini Serikali imewaongezea posho wabunge lakini kwetu madaktari hata kulipwa mishahara?. Kwanza hata dola yenyewe inazidi kuporomoka kila siku, lakini haitujali”, alisema Dk. Godfrey Mbawala.
Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza