Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuwapatia wananchi wote maji safi na salama. Imejiwekea malengo ya kuhakikisha ifikapo 2020 watu milioni 24 wapate maji ya uhakika ili kuwalinda dhidi ya magonjwa ya mlipuko na mabadiliko ya tabia nchi. Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ni kuwafikia watu bilioni 1.4 duniani kote kwa maji safi ifikapo 2030.
Malengo ya serikali ni utekelezaji wa matakwa ya Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 ambayo inaitaka serikali kutambua kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu, utoaji wa huduma ya maji vijijini na mjini uimarishwe.
Malengo ya serikali yanatokana na hali halisi ya tatizo la uhaba wa maji ambalo linaendelea maeneo mbalimbali nchini na kuathiri shughuli za uzalishaji mali na kuelekea uchumi wa viwanda na kati ifikapo 2025.
Kulingana na takwimu za shirika la Water Aid Tanzania (2017) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 26 nchini Tanzania na milioni 844 duniani kote hawapati maji safi na salama. Kwa muktadha mkakati wa serikali utapunguza tatizo kwa sehemu ikizingatiwa kuwa idadi ya watu nchini inaongezeka kwa kasi huku jitihada za kupunguza tatizo zikisuasua.
Katibu Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza hivi karibuni katika kipindi cha runinga alikiri kuwepo kwa uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.
“Maji tuliyonayo katika nchi hayaongezeki wakati idadi ya watu inaongezeka, lakini pili kwasababu ya shughuli zetu za kibinadamu tumeathiri baadhi ya vyanzo vya maji,” alinukuliwa Prof. Mkumbo.
Kijiji cha Nang’awanga kilichopo kata ya Njengwa Halmashauri Nanyamba iliyopo mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa vijiji vingi nchini ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya maji ya bomba na kuwalazimu wakazi wake kutumia maji ya visima vifupi ambavyo havikidhi mahitaji yote katika kijiji hicho.
Hata hivyo, maji hayo sio salama ambapo wanachi hutembea umbali mrefu kufuata maji safi katika vijiji vya jirani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Sera ya Taifa ya Maji 2002 inathibitisha kuwa “Matumizi halisi ya maji vijijini ni kati ya lita 5 kwa mtu kwa siku katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji, na lita 30 kwa mtu kwa siku kwa maeneo mengine. Kwa ujumla, maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ambayo mara nyingi siyo salama, hupatikana mbali na makazi ya watu”.
Mkazi wa Kijiji cha Madoto, tarafa ya Kimamba wilaya ya Kilosa, Joel Ndomembo anasema kwenye kijiji chao kuna zaidi ya visima viwili lakini havikidhi mahitaji ya wakazi wote, “serikali imejenga visima hapa kijijini lakini maji hayatoshi na tunalazimika kuyafuata kijiji cha jirani ambako ni zaidi ya kilomita 2”.
Mtoto akichota maji bombani
Mkakati wa Serikali
Licha ya serikali kutekeleza miradi ya maji vijijini imekuwa ikiendelea kupungua na mahali pengine miradi kutofanya kazi kabisa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo kutosimamiwa vizuri na kukosa matengenezo muhimu. Katika baadhi ya maeneo, watumiaji wa maji wengine bado wanadhani kuwa jukumu la kuwapatia wananchi huduma ya maji ni la Serikali pekee, kama ilivyokuwa hapo awali.
Serikali imeanzisha program maalumu ya uundwaji wa vyombo vya watumiaji maji (registration of legal community owned water supply organizations) katika maeneo ya vijijni ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kushirikishwa katika uendelezaji wa rasilimali hiyo muhimu nchini na kuachana na dhana ya kuisubiri serikali kuwapelekea maji.
Programu hii inahusu ujenzi wa miundombinu ya maji vijijini, uhamasishaji wa wananchi kuhusu usafi wa mazingira vijijini, na uimarishaji wa Halmashauri na taasisi mbalimbali. Utekelezaji wa programu unahusisha taasisi mbalimbali, zikiwa katika ngazi ya taifa, mikoa, Halmashauri, vijiji, na sekta binafsi. Ngazi ya mkoa inafuatilia na kutoa ushauri kwenye Halmashauri. Ngazi ya Halmashauri ndio nguzo kuu ya utekelezaji.
Lengo kuu la kuanzisha vyombo vya watumiaji maji ni kuifanya miradi imilikiwe na kusimamiwa na wananchi wenyewe ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji inakuwa endelevu. Ili miradi ya maji iwe endelevu na iweze kutoa huduma ya maji kwa ufanisi ni lazima iwe na fedha za kujiendesha zitakazotokana na mauzo ya maji.
Hii itawezesha huduma ya maji kuwa endelevu. Sera ya maji inasisitiza miradi ijengwe, iendeshwe na kusimamiwa na wananchi ili ijiendeshe kwa kufanya matengenezo kila inapohitajika bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.